Simba yaishtukia De Agosto, Banda arejea




HUKU winga hatari wa Simba, Peter Banda, akirejea rasmi na kuungana na wenzake kikosini akitoka chumba cha majeruhi, uongozi wa klabu hiyo umewashtukia wapinzani wao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Primeiro de Agosto...

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.
...na kuwataka wachezaji kuingia kambini mara moja kuepuka yasije yakawakuta ya msimu uliopita dhidi ya Jwaneng Galaxy FC ya Botswana.

Katika hatua kama hiyo ya Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy, huku wakiamini wamemaliza kazi na kilichobaki ni kukamilisha tu ratiba nyumbani, mechi ya marudiano Uwanja wa Benjamin Mkapa wakaachwa mdomo wazi baada ya kubugizwa 3-1 na timu hiyo ya Botswana kutinga hatua ya makundi.

Tayari Simba hadi sasa ina ushindi wa mabao 3-1 iliyoupata ugenini nchini Angola dhidi ya Primeiro de Agosto, hivyo mechi ya marudiano Jumapili wiki hii katika Uwanja wa Mkapa, inahitaji sare yoyote ama kutokubali kufungwa zaidi ya mabao 2-0 ili kufuzu hatua ya makundi, jambo ambalo uongozi unaepuka kujiaminisha kwamba wamemaliza kazi.

Hivyo, kuelekea mchezo huo kikosi cha Simba kimeingia kambini baada ya mazoezi ya jana jioni ili kujiandaa vema kwa mechi hiyo itakayopigwa Jumapili majira ya saa 10 alasiri.


Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema maandalizi yameanza rasmi jana katika Uwanja wa Mo Arena kujiandaa dhidi ya De Agosto, kuhakikisha wanapata ushindi ili kufuzu kucheza hatua ya makundi.

Alisema wameshinda ugenini lakini hawajafuzu na wanaendelea na maandalizi kwa ajili ya kufikia malengo yao ya kucheza hatua ya makundi na baada ya hapo kusonga mbele zaidi.

"Ushindi wetu ugenini dhidi ya De Agosto umetukumbusha msimu uliopita tuliopotolewa katika hatua hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi Jwaneng Galaxy.


"Mechi hiyo inatukumbusha msimu uliopita hatutaki kurudia makosa hayo, tumeshinda bao 3-1 ugenini, haijatufurahishwa kwa sababu imetukumbusha msimu uliopita, sasa tunaenda kama hatukucheza mechi ya kwanza," alisema Ahmed.

Alisema kiwango walichokionyesha dakika za mwisho zimewashtua na wanatolea macho kweli mechi hiyo kwa kupambana na kuhitaji kufuzu kwa matokeo mazuri mengine na si kutegemea yale ya Angola.

Ahmed alisema baada ya mapumziko ya siku moja waliyopewa wachezaji waliporudi kutoka Angola walianza mazoezi na jana jioni waliingia kambini moja kwa moja.

"Tumejipanga kuingia katika mchezo wa Jumapili bila kuangalia matokeo mazuri ya mechi ya kwanza, hatutaki kwa sababu yoyote itufanye tukose kufuzu hatua ya makundi," alisema meneja huyo.


Alisema hawatadharau na kuridhika na ushindi wa Angola, hivyo watashuka dimbani kwa tahadhari kubwa na kutowachukulia poa wapinzani wao katika mchezo wa Jumapili.

"Tunaingia kivingine, tunahitaji kufuzu...tunaenda kucheza mchezo huu kana kwamba hatujacheza mechi ya awali, tumekumbuka kucheza makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Lazima tuwe makini, lakini kuna taarifa njema kwa mashabiki wetu kurejea kikosini kwa Peter Banda, amefanya mazoezi na atakuwa sehemu ya mchezo wa Jumapili, kuhusu Shomari Kapombe anaendelea kufanya mazoezi hospitali, baada ya De Agosto atakuwa vizuri na kuanza kuonekana mechi za Ligi Kuu," alisema Ahmed.

Alisema wageni wao wanatarajiwa kuingia nchini Ijumaa mchana pamoja na waamuzi wanaotokea Afrika Kusini huku kamishna wa mchezo akitarajiwa kutua leo.


"Alhamisi tukiwa na hamasa katika Uwanja wa Mo Simba Arena, hapo mashabiki watapata nafasi ya kuona timu ikifanya mazoezi na siku ya Jumapili kutakuwa na burudani uwanjani kabla ya mchezo na kila shabiki atapewa bendera kwa ajili ya kuhakikisha wanapeperusha uwanjani wakati tunampelekea pumzi ya moto De Agosto," alisema.




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad