UNAAMBIWA wakati mashabiki wa Simba wakiendelea kushangilia ushindi wa mabao 3-0 walioupata timu yao dhidi ya Dodoma Jiji, tayari mabosi wa klabu hiyo, wametanguliza mashushushu wao nchini Angola ili kuwasoma wapinzani wao, Clube Desportivo 1º de Agosto.
Oktoba 8, mwaka huu, Simba itakuwa ugenini nchini Angola kuwakabili Clube Desportivo 1º de Agosto ikiwa ni mchezo wa kwanza raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Baada ya hapo, marudiano ni Oktoba 16, jijini Dar.
Chanzo chetu kutoka Simba, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, tayari kuna viongozi wameshatangulia nchini Angola, ili kuweka mambo sawa kabla ya kikosi chote kuwasili, huku ikiwa tayari wameshafanyia kazi baadhi ya mambo muhimu waliyokuwa wakiyahitaji
“Tunamshukuru Mungu, hadi sasa tumeshajua baadhi ya mbinu za wapinzani wetu na kwamba tunatengemea hadi kikosi kinapofika nchini Angola, hakitakumbana na changamoto yoyote ya kuhujumiwa, maana watu wetu wa kuandaa mazingira wameshaingia huko na kushughulikia mambo yote muhimu.
“Tunashukuru sana kufahamu baadhi ya mambo ambayo yatalisaidia zaidi benchi la ufundi katika mchezo huo, ambao kwa kiasi fulani mazingira yapo sawa na kwamba tutacheza bila presha kwani tumeshategua mitego yao mingi waliyokuwa wamejiandaa nayo,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wa Meneja wa Habari na Mawasilioni wa Simba, Ahmed Ally alisema: Ni kweli tayari kuna watu walienda Angola tangu wiki iliyopita na kwamba tayari amerudi baada ya kuweka mambo yote sawa, hivyo hatuna shaka ya lolote kutokea huko,” alisema Ahmed Ally.
STORI: MUSA MATEJA