BAO pekee lililofungwa na Moses Phiri lilitosha kuivusha Simba hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika wakiungana na Vipers walioing’oa TP Mazembe.
Simba wametinga hatua hiyo baada ya ushindi wa mabao 3-1 ugenini na leo kupigilia msumali kwa kupata ushindi wa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilikuwa bora kwa timu zote kuonyeshana ubora wa kuchezea mpira huku wenyeji wakisaka bao la kuendelea kuongoza na De Agosto wakitafuta bao la kusawazisha.
Timu zote zilifanya mabadiliko lakini hayakuwa na faida kwa pande zote mbili kutokana na kushindwa kuongeza bao, De Agosto ilifanya mabadiliko kwa wachezaji wake watano.
Kwa upande wa Simba, Mgunda alifanya mabadiliko kwa wachezaji watatu akimtia Sakho, Okra, Tshabalala, Israel na Phiri nafasi zao zilichukuliwa na Gadiel Michael, Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Habibu Kyombo na Denis Kibu.
Ushindi wa Simba umewafanya watinge hatua ya makundi kwa idadi ya mabao 4-1 na kuwafanya mashabiki wao washindwe kujizuia kwa shangwe.
Shabiki amvaa Kanoute
Katika hali ya kushangaza shabiki ambaye hakutambulika ni wa timu gani kutokana na kuwa kifua wazi aliingia uwanjani na kumkumbatia kiungo wa Simba Sadio Kanoute.
Kiungo huyo ambaye alikuwa uwanjani akipasha misuli moto kwaajili ya kuendelea na mechi kipindi cha pili alivamiwa na shabiki huyo na kumkumbatia.
Walinzi waliokuwa uwanjani waliingia na kumtoa kwa nguvu wakimbeba juu na kumtoa nje ya uwanja.