LICHA ya kwamba wapo kambini, lakini mapumziko ya leo ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa yamezikuta vizuri familia za mastaa wa Simba itakayomalizana na Primeiro de Agosto Jumapili, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kishindo cha tajiri wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ akiwa sambamba na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ kimezikumba akaunti za mastaa hao baada ya kujazwa mkwanja. Mo ambaye alikuwa kimya kwa muda akiacha majukumu kwa wasaidizi wake, amewalipa bonasi zote alizokuwa amewaahidi tangu kwenye mechi ya ugenini dhidi ya Nyasa Big Bullets. Mkwanja huo umeongeza mzuka mkubwa kambini na wamegawiwa kwa vigezo walivyojiwekea.
Aliyecheza mechi nyingi kama Clatous Chama, Moses Phiri, Aishi Manula na wengine watapata mgao mkubwa tofauti na wale waliocheza michezo michache kama Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Nelson Okwa na wengine.
Twende sawa. Siku mbili kabla ya Simba kwenda Angola katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Agosto wachezaji na benchi la ufundi wote walilipwa mishahara yao ya mwezi Septemba.
Mo Dewji akishirikiana na Try Again hawakuishia hapa juzi Jumatano jioni akawalipa wachezaji na benchi la ufundi bonasi za mechi tano mfululizo ambazo walipata ushindi kwenye Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Bonasi ya kwanza ilikuwa Sh200 milioni baada ya kushinda ugenini mabao 2-0 dhidi ya Nyasa Big Bullets. Bonasi nyingine ni Sh20 milioni ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Prisons Uwanja wa Sokoine Mbeya.
Baada ya hapo Simba ilipata ushindi nyumbani 2-0 dhidi ya Nyasa Big Bullets na kuwaondoa kutokana na ushindi huo wamelipwa bonasi ya Sh100 milioni.
Ushindi wa mabao 3-0, dhidi ya Dodoma Jiji bonasi iliyowekwa kwa wachezaji na benchi la ufundi Sh20 milioni kama ilivyo kawaida wakishinda mechi ya ligi tofauti na zile dhidi ya Yanga na Azam hiyo ndio huchukua ila wakitoka sare au kufungwa hawapati kitu.
Siku moja kabla ya kucheza dhidi ya Primeiro de Agosto, wachezaji na benchi la ufundi waliahidiwa bonasi ya Sh200 milioni na watapewa kabla ya mchezo wa marudiano.
Mo Dewji na viongozi wa Simba watatembelea kambi ya timu yao siku moja kabla ya kucheza mechi ya marudiano na Agosto tayari wamewaeleza kama watashinda wachezaji na benchi la ufundi watapewa bonasi ya Sh100 milioni wataipata kabla ya kucheza mchezo wa kwanza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Kinara wa mabao kwenye kikosi cha Simba katika Ligi ya mabingwa Afrika, Phiri alisema kwenye timu nyingi alizopita suala hilo na bonasi linakuwepo ili kuongeza morali na hali uashindani kwa wachezaji.
Meneja wa habari Simba, Ahmedy Ally alisema maandalizi ya timu yao yanakwenda vizuri ili kuhakikisha wanakwenda kupata ushindi na kuweka historia nyingine kubwa ya kutinga hatua ya makundi.
“Viongozi tunaendelea kutimiza majukumu yetu ili kuhakikisha wachezaji na benchi la ufundi wanakuwa kwenye mazingira sahihi ya kufikilia mchezo zaidi na kutimiza lengo letu kuu la kushinda,” alisema Ally.