Takribani watu 150 wamekufa katika wilaya ya Itaewon mjini Seoul nchini Korea Kusini sehemu ambayo ni maarufu kwa burudani za usiku na kutembelewa zaidi na vijana na wageni huku ikiwa imesheheni migahawa na sehemu za burudani ambapo mkanyagano ulitokea wakati wa kusherekea sikuku ya Halloween oktoba 29, 2022.
Rais wa nchi hiyo Yoon Suk-yeol, ameamuru maafisa kupeleka timu za huduma ya kwanza na kuweka tayari vitanda hospitalini kwa walioathirika huku Meya wa Seoul Oh Se-hoon, ambaye alikuwa ziarani barani Ulaya, amelazimika kukatisha ziara yake, kulingana na shirika la habari la Korea Yonhap.
Kwa mujibu wa maafisa wa zimamoto wamesema watu waliendelea kumiminika kwenye uchochoro mwembamba ambao tayari ulikuwa umefurika ukuta hadi ukuta, wakati wengine waliokuwa juu ya barabara yenye mteremko wakianguka na kuwaangusha wengine.
Afisa wa idara ya Zimamoto Choi Seong-beom amesema “idadi kubwa ya majeruhi ilitokana na wengi kukanyagwa wakati wa sherehe za Halloween,” akiongeza kwamba idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters shuhuda mmoja aliyejulikana kwa jina la Monn Ju-Young amelieza shirika hilo kuwa “kulikuwa na dalili zote kwamba kutakuwa na tatizo kwenye uchochoro kabla ya tukio”.
Baadhi ya mashuhuda wengine wameelezea matukio ya ghasia muda mfupi kabla ya kutokea mkanyagano, huku polisi waliokuwa wakifuatulia sherehe hizo za Halloween wakishindwa kudhibiti umati mkubwa wa watu.
Picha za kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha mamia ya watu wakiwa wamejazana kwenye kichochoro chembamba kilicho kwenye mteremko huku polisi na maafisa wa msaada wa dharura wakijaribu kuwavuta na kuwatoa.
Picha nyingine zimeonesha matukio ya maafisa na raia wakiwapatia huduma ya kwanza watu wengi ambao walionekana kupoteza fahamu.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ametuma salamu za rambirambi kufuatia mkasa huo wa Korea Kusini, ambapo amesema “ni tukio la kutisha huko Seoul na imetushtua sisi sote.”
Rais wa Marekani Joe Biden amesema Marekani “inasimama pamoja” na Korea Kusini kufuatia mkanyagano uliosababisha vifo vya watu kwenye sherehe za Halloween katika mji mkuu wa nchi hiyo ambao umeua takriban watu 150.