KAMATI ya Uendeshaji na Usimamisi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imemfungia michezo mitatu na kulipa faini ya shilingi milioni moja, golikipa wa timu ya Singida Big Stars, Metacha Mnata kwa kosa la kumpiga kwa makusudi straika wa Mtibwa Sugar, Charles Ilamfya.
Katika kikao chake cha Oktoba 24, pamoja na kuamua mambo mbalimbali ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Championship, kamati hiyo imefanya maamuzi hayo kwa kuzingatia kanuni zinazoongoza mchezo huo.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi, imesema kuwa kamati hiyo imemkuta na hatia kipa huyo kumpiga mchezaji wa timu pinzani kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa uwanja wa Manungu Complex, Oktoba 18, mwaka huu na Mtibwa ikashinda kwa bao 1-0.
Kamati hiyo pia imeipiga faini ya shilingi milioni moja Klabu ya Prisons baada ya mashabiki wake kuwatolea lugha ya matusi wasimamizi wa mchezo kati ya timu hizo mbili uliochezwa Oktoba 9, kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro.
Hali hiyo ilitokea baada ya mashabiki hao kutaka kuingia uwanjani bure, bila ya kukata tiketi, timu hizo zikitoka suhulu.
Pia, kamati hiyo imemfungia miezi mitatu na kumtoza shilingi laki tano kocha wa makipa na Namungo FC, Farouk Ramadhani baada ya kuwatolea lugha ya matusi watoto waokota mipira wa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Imedaiwa kuwa kipa huyo wa zamani wa Simba katikati ya miaka ya 1990, alikuwa akiwashutumu watoto hao kuwa walikuwa wanachelewesha kurudisha mipira uwanjani kwa makusudi.
Kwenye mechi hiyo iliyochezwa Oktoba 19, Polisi Tanzania ikiwa wenyeji, Namungo ilipoteza kwa bao 1-0.