KWA miaka mingi baadhi ya wasanii wa Bongofleva wamekuwa na utamaduni wa kuanzisha uhusiano wa kimapenzi kwa lengo la kujenga familia lakini hasa inadaiwa wengi wao hufanya hivyo ili kuchukua usikivu wa mashabiki na kuinuana kimuziki.
Hilo hutoa fursa kwa wahusika kuingia studio na kurekodi nyimbo ambazo hubaki kama alama ya penzi lao hata pale ambapo wameachana. Hawa ni baadhi tu ya wasanii ambao muziki wao mzuri umebaki ila uhusiano, hapana!.
1. Diamond X Tanasha - Gere
Katika Extended Play (EP) yake, DonnaTella yenye nyimbo nne, Tanasha Donna kutokea nchini Kenya alimshirikisha Diamond Platnumz aliyekuwa mpenzi wake katika wimbo, Gere uliofanya vizuri Afrika Mashariki.
Mara baada ya wimbo huu kutoka Februari 18, 2020, tetesi za uhusiano kuvunjika zikaanza kushika kasi kwenye mitandao, wiki kadhaa mbele Tanasha akathibitisha kuachana kwao wakiwa tayari na mtoto mmoja.
2. Vanessa Mdee X Jux - Juu & Sumaku
Kwa mara ya kwanza walikutana studio, B’Hits Music Group na aliyewakutanisha ni marehemu Prodyuza, Pancho Latino, kutokana na hilo, ndio sababu kwao wao kuweza kushirikiana vilivyo katika muziki.
Penzi likamelea, wakatoa wimbo wa pamoja, Juu, chini ya Prodyuza Luffah, ukafanya vizuri kwa kiasi chake. Waliachana na kurudiana, wakaamua kurudi tena studio na kurekodi wimbo mwingine, Sumaku ambao ulitoka wakati mapenzi yao yanafikia ukingoni kabisa.
3. Lord Eyes X Ray C - Kwa Ajili Yako
Mapenzi yao yalianza kipindi Lord Eyes anafanya vizuri na kundi la Nako 2 Nako Soldiers kabla ya sasa anapotamba na kundi la Weusi, Ray C naye alikuwa kwenye kilele cha mafanikio ya muziki wake upande wa uimbaji.
Wakati penzi likipamba moto waliachia wimbo matata, Kwa Ajili Yako ukitayarishwa chini ya studio za Mandugu Digital, pia alisikika Ibra da Hustler kwa sababu ulikuwa ni wimbo wa kundi. Julai 2009 ndipo Ray C alidokeza kuwa wameachana, hata hivyo tetesi za kurudiana zilizidi kuchukua nafasi lakini haikuwa hivyo.
4. Shilole X Nuh Mziwanda - Ganda la Ndizi
Kipindi cha uhusiano wao kabla ya kurekodi wimbo wao, Shilole alitokea kwenye video ya wimbo wa Nuh Mziwanda, Msondo Ngoma uliotoka mwaka 2014.
Waliamua kuunda kundi lao na kulipa jina la ‘Shiwonder’ ikiwa ni muunganiko wa majina yao na kisha kutoa wimbo wa kwanza, Ganda la Ndizi. Wimbo huo ulitoka mara baada ya kuwepo tuhuma za kuwa Nuh analelewa na Shilole kitu kilichosababisha kuvumilia vipigo vya kila mara.
5. Lady Jaydee X Spicy Music - Together Remix
Wakati Spicy Music kutokea Nigeria anatamba chini ya lebo ya Mr. Flavour, 2nite Music Group, ndipo uhusiano wake na Lady Jaydee ulichukua nafasi ukiwa ni wa kwanza kwa Jide kuuweka wazi tangu kuvunjika kwa ndoa yake. Haikuchukua muda wakatoa wimbo, Together Remix uliofanya vizuri sana, ni wimbo ambao Spicy ameuandika na kuutayarisha mwenyewe japo kwenye verse ya Jaydee alilazimika kuzitafsiri na kuziboresha kwa lugha ya Kiswahili. Waliachana kimya kimya sana bila drama kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya mastaa duniani kote.
6. One The Incredible X Grace Matata - Salamu & Light It Up
Ukaribu wao ulianza wakati wanafanya muziki pamoja chini ya lebo ya M Lab (Music Laboratory) na ndipo walipoanza kufahamika zaidi ndani ya kiwanda cha muziki wa Bongofleva. Walikuwa na uhusiano lakini ulioghubikwa na usiri mkubwa.
Hadi sasa nyimbo walizotoa pamoja ni kama ‘Salamu’ na ‘Light It Up’ unaopatikana kwenye albamu ya One The Incredible, R.A.P (Representing Africa Popote) iliyotoka Desemba 2014. Wenyewe walisema uhusiano wao ni maisha binafsi, hivyo mashabiki wao wajikite kufuatilia muziki wao.
7. Izzo Bizness X Abela Music - Dangerous Boy, Umeniweza &
Tumeoana
Wawili hawa waliunda kundi lijulikanalo kama ‘The Amazing’ katikati ya mwaka 2016, Abela Music ni mwimbaji aliyekuwa na makazi yake nchini Marekani mwenye asili ya Bukoba, Tanzania.
Mara baada ya kuunda kundi wimbo wao wa kwanza kuutoa ni Dangerous Boy, kisha wakatoa nyingine zilizofanya vizuri kama Umeniweza na Tumeoana. Kipindi chote walikana tetesi za kuwa na uhusiano lakini baada ya Abela kujifungua wawatoto mapacha Aprili, 2018 akiwa Marekani ndipo ikathibitika walikuwa wapenzi ila sasa hawapo pamoja.
8. Amini X Linah - Mtima Wangu
Mara baada ya kupikwa ndani ya Tanzania House of Talent (THT), wakawika vilivyo ndani ya Bongofleva na wimbo wao wa kwanza kama wapenzi unaokwenda kwa jina la Mtima Wangu.
Waliachana na kila mmoja kuwa na uhusiano mpya, hata hivyo hilo halikuwa kikwazo kwa wao kurejea studio na kutoa wimbo mwingine, ‘Nimenasa’ ambao uliibua vikali hisia za wawili hao kurudiana lakini haikuwa hivyo hadi sasa.
9. Kusah X Ruby - Kelele, Chelewa & Nadondosha
Uhusiano wao ulikuwa ni mwanzo kuinuana kimuziki kutokana Ruby ni mwimbaji mzuri wa studio na jukwaani, huku Kusah akiwa ni mwandishi mzuri wa nyimbo na ameshawaandikia wasanii wengi. Kwa kipindi walichokuwa wote walitoa nyimbo tatu ambazo ni Kelele, Chelewa na Nadondosha, baada ya nyimbo hizo ukawa mwisho wa penzi lao wakiwa tayari wamejaliwa kupata mtoto mmoja. Inaelezwa ugomvi wao hadi kuachana ulianzia studio.