Upelelezi kesi ya Sabaya bado



Moshi. Wakati aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akiendelea kusota mahabusu kwa siku 132 sasa tangu afikishwe mahakamani, mwendesha mashtaka wa Serikali, Kassim Nassir amesema upelelezi wa kesi hiyo utakamilika ndani ya siku 90.

Katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2022, Sabaya anakabiliwa na mashtaka saba likiwamo la uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka, kuomba na kupokea rushwa ya Sh30 milioni kutoka kwa mfanyabiashara wa Bomang’ombe, Alex Swai aliyemtuhumu kukwepa kodi.

Juni Mosi, mwaka huu, Sabaya na wenzake wanne walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Moshi wakikabiliwa na mashtaka hayo na Septemba 6, Mahakama iliwaachia huru washtakiwa wanne, ambao ni Sylivester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey baada ya kukiri kutenda makosa na kutiwa hatiani.

Mahakama iliwaamuru kulipa kila mmoja faini ya Sh50,000 na fidia ya Sh1 milioni kwa mwathirika wa tukio hilo ambaye ni Alex Swai.


Awali, wakili wa upande wa utetezi, Hellen Mahuna aliieleza Mahakama kuwa, kesi inayomkabili mteja wake (Sabaya), imekaa kwa siku 132 bila upande wa mashtaka kueleza chochote kinachoeleweka zaidi ya kusema upelelezi bado haujakamilika.

Hivyo, aliiomba Mahakama hiyo itumie hekima na mwongozo uliotolewa na DPP kuifuta kesi hiyo.

“Mheshimiwa kesi hii imeshakaa kwa siku 132, upande wa jamhuri hawajatuambia chochote kinachoeleweka zaidi ya kusema upelelezi haujakamilika na kuomba kesi ipangwe tarehe nyingine.


“Wanachofanya mawakili wa Serikali ni kinyume na utaratibu, kwa sababu wanaenda kinyume na mwongozo waliopewa na DPP, hawakamilishi upelelezi kwa wakati na wanamweka mshitakiwa ndani na kumnyima haki zake za msingi,” alieleza wakili Mahuna.

Aliiomba Mahakama iangalie na itumie hekima kutoa mwongozo unaostahili huku akidai kinachofanywa na upande wa mashtaka ni kinyume na utaratibu wa ofisi ya DPP iliyotolewa mwongozo kwamba upelelezi wa kesi unatakiwa umalizike ndani ya siku 90.

Wakili upande wa mashtaka, Suzy Kimaro aliieleza Mahakama kuwa mwongozo uliotolewa na DPP umeanza kutumika Oktoba mosi, mwaka huu, hivyo hawako nje ya muda tangu mwongozo huo utolewe.

“Wakili wa utetezi anapoleta hii hoja ni kwamba inazua hoja nyingine, mwongozo huu umeanza kutumika Oktoba mosi mwaka huu,hivyo hatuko mbali na muda wa maelekezo yaliyotolea na DPP na hatujapitwa na wakati na hatujakiuka taratibu zozote,” alisema.


Mwendesha mashtaka wa Serikali, Kassim Nassir alisema kwa kuwa mwongozo huo umeanza kutumika Oktoba mosi na ni siku 10 tu zimepita, shauri hilo litakamilika ndani ya siku 90.

Hata hivyo, Hakimu mfawidhi mkazi wa Mahakama hiyo, Salome Mshasha alisema, “mwongozo huu uanze kutumika kama ilivyoelekezwa Oktoba mosi mwaka huu, hivyo tunaahirisha shauri hili mpaka hapo upelelezi ndani ya muda ambao umeelekezwa, kesi hii itatajwa tena Oktoba 24 na mshtakiwa ataendelea kuwa chini ya ulinzi wa magereza akisubiri upelelezi ukamilike.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad