Utata mkubwa kifo mwanamke anayedaiwa kujinyonga Tabata
Wingu zito limeendelea kutanda miongoni mwa wanafamilia, ndugu na majirani juu ya kifo cha Piarisi Hiza, anayedaiwa kujinyonga nyumbani kwake Tabata jijini hapa.
Piarisi Hiza alikuwa mama wa watoto wawili, wa kiume akiwa na umri wa miaka mitatu na wa kike akiwa na miezi tisa, alipoteza maisha Jumapili ya Oktoba 2, 2022 ndani ya chumba alichokuwa amelala na mume wake.
Mazingira ya kujiua kwake ndiyo hasa yaliyoacha maswali kwa ndugu, majirani na watu wa karibu, huku baadhi wakihisi huenda ameuliwa.
Akizungumzia hatua walizochukua kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema bado wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.
“Tunachunguza mambo mengi, mtu akifa huenda kukawa na chanzo chake kwani siyo kila anayekufa ameuliwa.” Kwa upande wa ndugu wa karibu wa marehemu, akisimulia namna alivyopata taarifa hizo kwa sharti la jina lake kutoandikwa gazetini alisema Jumapili saa tano asubuhi alipigiwa simu na ndugu zake waliopo Lushoto, mkoani Tanga, wakimtaka kufika nyumbani kwa dada yake wakidai amejiua.
“Nililazimika kukata simu ya Lushoto na kumpigia dada wa kazi (Aneth) nikamuuliza imekuwaje akaniambia marehemu na mumewe walitoka siku ya Jumamosi usiku kwenda sehemu za starehe na walirudi Jumapili asubuhi na kupitiliza chumbani kulala. “Niligongewa mlango na mume wa marehemu (John) na kuniambia dada amejinyonga chumbani. “Nilipiga kelele zilizosababisha majirani kujaa ili kujua kuna nini.”
Alisema alipopata maelezo hayo alipanda bodaboda ili awahi sehemu ya tukio, Tabata Segerea ambapo alikuta marehemu amelazwa chini, lakini alipomkagua hakuona alama yoyote iiliyoashiria mtu kujinyonga, ikiwamo shingoni kutokuwa hata na mkwaruzo.
“Sasa hatuelewi, huenda alimsukuma kwa bahati mbaya akagonga kichwa, siwezi kuthibitisha hili kwa sababu alikuwa na nywele ndefu hivyo ni ngumu kuona kama ameumia kichwani, kujinyonga siyo rahisi kwa sababu pia wote walikuwapo chumbani, haiwezekani aseme alikuwa amelala hadi mtu anamaliza kujinyonga ndiyo ushtuke.
“Hata feni anayodaiwa kuitumia kujinyonga si rahisi kwa sababu marehemu alikuwa na uzito mkubwa ambao kitu kigumu ndiyo kingeweza kuhimili,” alisema.
Akizungumza na gazeti hili, Aneth ambaye ni binti wa kazi aliyekuwapo nyumbani siku ya tukio alisema: “Sikuwa najua chochote, nilipewa taarifa na John, mume wa marehemu,” alisema binti huyo akiwa amemshika mtoto mkubwa wa marehemu mwenye miaka mitatu ambaye alikuwa akicheza huku na kule katikati ya waombolezaji, lakini ilifika wakati aliuliza kuhusu alipo mama yake.
“Mama amekwenda sokoni atakuja muda si mrefu,” mmoja wa ndugu wa marehemu alimwambia mtoto huyo aliyeridhika na jibu na kuendelea na shughuli zake.
Mmoja wa majirani ambaye pia hakutaka jina lake liandikwe gazetini aliyekuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika baada ya kusikia kelele alisema:
“Nilipofika sikuona dalili ya kinachoelezwa na mwanaume, mtu kajinyonga lakini hakuna hata stuli wala kiti ndani ambacho tuseme alikitumia kama nyenzo ya kupanda ili kufikia feni, pia inaonekana tukio lilitokea zamani siyo la muda ule, kwani tulipofika mwili wa marehemu ulikuwa umeshaanza kukauka.