Vituko, historia ya sanamu la 'Bismin'



MAKUTANO ya barabara ya Samora na Azikiwe, mitaa ya Posta kuna sanamu moja kubwa jeusi lililo juu kwa jukwaa au jiwe kubwa.
Adam Fungamwango

Sanamu ya askari mweusi kuwakilisha mwafrika aliyepigana vita kuu ya kwanza ya dunia lililopo maeneo ya Posta Dar es Salaam maarufu kama ‘picha ya Bismin’. 

Sanamu inamuonyesha mtu mweusi akiwa amevaa shati na kaptula, ameshika bunduki.Sanamu hiyo imeupa mgongo upande wa Magharibi na bunduki yake imeelekezwa upande wa Mashariki, baharini ambako inatoka kuelekea barabara ya Azikiwe, huku ya Samora ikiwa inapita ubavuni mwake. 

Eneo la mduara ambapo magari yanapita kushoto kila upande, katikati yake kuna bustani ndogo.Kwa miaka ya hivi karibuni naona kama kizazi cha sasa hakifuatilii au kutaka kujua historia ya sanamu hilo, siyo kwa nini limewekwa pale tu, lakini lilivyokuwa likitetemesha watu wengi, hasa waliokuwa wanatoka mikoani.Miaka ya 1990 kurudi nyuma, sanamu hilo lilikuwa maarufu zaidi Dar es Salaam kuliko kitu chochote kile.

Hadi leo inabaki kuwa ndiyo nembo ya Dar es Salaam. Ukiwa unaiongelea Dar hata kwenye televisheni bila kuonyesha sanamu hiyo inakuwa kama hujaiongelea vizuri.Watu waliokuwa wanatoka mikoani na kufikia kwa ndugu zao moja ya sehemu ambazo walikuwa wanaomba wapelekwe ni kuiona sanamu hiyo ambayo ilijichukulia umaarufu mkubwa nchini.Miaka hiyo sijui kwa nini walikuwa hawaiiti sanamu ya Bismin, ila ilijulikana kama 'picha ya Bismin.

'Kwa miaka hiyo hakuna mtu yoyote kutoka mikoani ambaye anaweza kuaminika kama amefika jijini Dar es Salaam kama hajaiona sanamu hiyo.Anaporudi kijijini na kuulizwa inabidi awe na ushahidi wa kutosha kama kweli alikwenda Dar kwa kujibu maswali kadhaa ambayo wenzake watathibitisha kuwa kweli amefika.Kufika Dar hasa kwa watu wa mikoani hakikuwa kitu cha mchezo mchezo hasa kutokana na miundombinu ya wakati huo. Dar ilionekana iko mbali mno, na pia ilionekana kama vile mtu anapokwambia anakwenda au anatoka Ulaya.Moja ya vitu ambavyo wengi waliofika Dar ambavyo wamekuwa wakiulizwa wanaporejea, na ndiyo wanavyotaka kupelekwa na kutembezwa na ndugu zao ni sanamu ya Bismin, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ambao kwa sasa unaitwa Julius Nyarere, Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Kivukoni, Hospitali ya Muhimbili, na klabu za Simba na Yanga.

Kwa uchache ukipata hata nusu ya hivi nilivyovitaja, na ukawa na ushahidi hata kama siyo wa picha ila maneno tu, ukajibu maswali yao vizuri, basi wewe kijijini utatamba na watu watakuheshimu kuwa umefika Dar es Salaam.Katika vitu vyote hivyo, ilikuwa rahisi sana kwa mgeni kumpeleka kwenye sanamu ya Bismin kwa sababu sehemu mabasi kutoka sehemu zote jijini yalikuwa yakiishia Kariakoo au Posta.

Sasa vituko vinakuja pale vijana au watoto watukutu wanapowapeleka wenzao wanaotoka mikoani kwenye sanamu hilo wanavyowatisha.Wanapofika pale wanawaambia waiamkie, la sivyo ile bunduki itafyatuliwa na kumuua. Hiyo ilisababisha wengi wakati huo waliorejea kijijini au waliobaki hapa hapa Dar, lakini waliotoka vijijini kuiamkia sanamu hiyo.Ni moja ya sanamu iliyopata 'shikamoo' nyingi wakati huo.

 Waliaminishwa kama sanamu ile ina uhai, na yule ndiye mwenye mji wa Dar es Salaam, asipomwamkia atapigwa bunduki au kurudishwa kijijini au mkoa aliotoka.Wengine walipigishwa magoti kabisa na kuambiwa amwambie 'mzee shikamoo' na wakafanya hivyo.Mbinu hiyo ilitumiwa na 'watoto wa mjini' kuwaingiza mjini waliotoka 'bushi' kwa sababu wengi wao inadaiwa walikuwa wakilizoea jiji wanajifanya wajuaji zaidi kuliko wenyeji.

Kwa hiyo huwa anakumbushwa kuwa asijifanye mjuaji sana au mjanja wakati wao ndiyo wamemuonyesha mji, kiasi kwamba walimpeleka hadi kwenye 'picha ya Bismin' na kuiamkia. Hiyo humfanya mjuaji anywee na kuwa baridi kama maji ya mtungini. Kwa nini sanamu ile imewekwa pale? Na ni nini? Na kwa nini ikawa ndiyo nembo ya Dar es Salaam?Historia yake inaanza mwaka 1889, kabla na baada ya Vita Kuu ya kwanza ya Dunia.

Kwa ufupi sanamu ya mwanzo kukaa pale ni sanamu ya Herman Von Wissman, Gavana wa Kijerumani ambaye anakumbukwa kwa kutekeleza utekaji na mauaji ya Abushir Ibn Salim Al Harthi, mtawala na sultaniwa Pangani Tanga.Baada ya kumteka na kumyonga Abushir, Von Wissman alirejea Ujerumani na kisha baadaye kuteuliwa kuwa Gavana wa Nchi zilizokuwa chini ya Ujerumani za Afrika Mashariki.

Alifanya utafiti wa kutafuta ni wapi kitovu cha mji wa Dar es Salaam, yaani katikati ya Dar es Salaam au Mzizima wakati huo tena kwa vipimo, ndipo alipogundua sehemu ile ndiyo katikati ya Dar wakati ule. Hii ina maana bado sehemu kubwa ya Dar ya sasa ilikuwa pori, nafikiri mwisho upande wa Magharibi ilikuwa ni Manzese, na Mashariki na kuvuka Kigamboni halafu kuna Kariakoo, Ilala, Magomeni, na Msasani.Wissman alisimamisha sanamu yake mwaka 1909, nadhani ndiyo maana wengi wakawa wanaifahamu kwa jina la 'picha ya Bismin' hasa Waswahili wakati huo, wakishindwa kutamka Wissman.Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia iliyopiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918, Waingereza walishinda na kuchukuwa koloni la Tanganyika, ndipo mwaka 1916 sanamu la Bwana Von Wissman liliondolewa na likawekwa Sanamu la sura ya askari mweusi Mwafrika katika sare ya kijeshi ya King's African Rifles wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-1918) akishika bunduki yenye kisu cha kando na kutazama upande wa bahari mwaka 1927 Hii ilikuwa ni kama ishara ya kuthamini Waingereza kutambua mchango wa Askari Waafrika waliopigana kwenye Vita hivyo. 

Sanamu imedumu hadi leo hapo panapoitwa Askari Monument Garden, Posta Dar es Salam.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad