Vyama 14 vyaishukia Chadema, nao wajibu




Dar es Salaam. Muungano wa vyama vya siasa vya upinzani 14 nchini umetangaza kuunga mkono ripoti Kikosi cha kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutafuta na kuchakata maoni ya wadau kuhusu mfumo wa demokrasia, huku wakikosoa msimamo wa Chadema kupinga ripoti hiyo.

Oktoba 21, kikosi hicho kilikabidhi ripoti yake kwa Rais Samia iliyokuwa na mapendekezo 18 katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Jana Oktoba 22 Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alitangaza msimamo wa chama hicho kwa waandishi wa habari wa kutoiunga mkono ripoti hiyo, huku akiitaka Serikali kuweka wazi gharama zilizotumiwa na kikosi hicho.

Mnyika pia alisema kuwa chama hicho bado kinaamini rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba mwaka 2014.


Tangu awali Chadema haikutaka kwenye mkutano wa Baraza la vyama vya siasa ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na kufanyikia Dodoma Desemba 2021 uliozaa kikosi hicho.

Leo Oktoba 23 vyama 14 vimeibuka jijini hapa na kukosoa msimamo wa Chadema vikisema chama hicho kingejipa muda wa kuitafakari ripoti hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya vyama hivyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Doyo Hassan Doyo amesema hawaungi mkono hoja zilizotolewa na Chadema na kwamba wamekurupuka kujenga hoja bila kufanya utafiti.


"Tumeisikiliza taarifa yao na kupitia kwa kina na kwa hakika tunachoweza kusema viongozi wa Chadema wamejawa ubinafsi choyo na wivu mkubwa kuona Tanzania inaweza ikawa katika maridhiano huku wao wakiwa nje ya mchakato huo," amesema.

Amesema Rais Samia baada ya kuingia madarakani kwa nafasi yake kama mkuu wa nchi, alitoa kipaumbele cha kutafuta suluhu ya kitaifa kwa kufanya vikao na wadau mbali mbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa kabla ya kuundwa kwa kikosi kazi hicho.

"Tunaendelea kusema Chadema imeonyesha ubinafsi wa hali ya juu katika kipindi ambacho tulipaswa kuwa pamoja.

“Ni wazi tunafahamu baada ya wadau wa siasa kukutana jijini Dodoma Chama hicho kilisusia vikao hivyo wakituhumu kuwa hawawezi kukaa meza moja na Msajili wa vyama vya siasa kutafuta muafaka," amesema.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema chama hicho kinaendelea na msimamo wake wa kupinga ripoti hiyoalipozungumza kwa simu leo.

“Tulitegemea hayo wangeyazungumza kwa wao ni sehemu ya Kikosi Kazi, kwa hiyo kutetea hoja yao haitushangazi.

“Mfano hata aliyekuwa mzungumzaji anatoka kwenye chama ambacho kiongozi wake alikuwa makamu mwenyekiti wa kikosi hicho, sasa ulitegemea wangeenda tofauti na hoja yao,” amesema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad