Mbeya. Mganga Mkuu wa Hosptali ya Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya, Diodes Ngaiza amesema, watu watano wamethibitika kufariki kutokanana na ajali kati ya basi la Kyela Express na basi dogo aina ya Toyota Coaster, huku majeruhi wakifikia 31.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumanne Oktoba 11, Dk Ngaiza amesema kuwa kati ya majeruhi hao, 14 walikimbizwa katika hosptali ya Mission Igogwe, huku 17 katika hosptali ya Wilaya ambapo watatu walipoteza maisha wakipatiwa matibabu na wanne wamepewa Rufaa katika hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH) kwa matibabu zaidi.
''Vifo vya watu watatu vimeongezeka kutokana na majeruhi 14 waliokimbizwa katika hosptali ya Mission ya Igongwe na hivyo kuongeza idadi ya vifo kutoka watu wawili waliofariki katika eneo la tukio na kufanya idadi ya vifo kuwa vitano,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dk Vincent Anney aliyetembelea eneo la ajali, amesema kuwa taarifa za awali zinaonyesha madereva wote wawili akiwemo dereva wa Coaster aliyemiongoni mwa waliofariki, akielezwa kuendesha kwa mwendo kasi na kutaka kulipita lori lililokuwa mbele yake na kusababisha kugongana uso kwa uso na basi la Kyela Express.
Ajali hiyo imetokea leo Jumanne Oktoba 11 majira ya saa 2.30 za asubihi katika kijiji cha Ibula Kata ya Kiwira iliyohusisha gari aina ya Costa iliyokuwa ikisafirisha msiba kutoka Dodoma kwenye Kyela mkoani hapa.