Wataalamu Waonya Upasuaji usio wa Lazima kwa Wajawazito





Katika siku za hivi karibuni kujifungua kwa upasuaji kumeonekana kama ‘fasheni’, kwani kuna idadi ya wanawake wengi wanaofika hospitali kuomba kupatiwa huduma hiyo bila sababu za kitaalamu.

Wataalamu wa afya wametaja sababu tatu za wanawake kuomba kujifungua kwa upasuaji, ikiwemo ile ya kutoharibu muonekano wa sehemu zao za siri, kuogopa maumivu ya uchungu, hasa kwa wanaojifungua kwa ujauzito wao wa kwanza na kuepuka maumivu mara mbili, kwani wanawake wengine huumwa uchungu na baadaye hutakiwa kufanyiwa upasuaji, hivyo hufanya maamuzi mapema.

Wataalamu wanasema sababu hizo hutokana na kuwepo kwa simulizi zinazotolewa kwenye vijiwe na baadhi ya wanawake huwatisha wasichana wadogo juu ya kuwepo kwa maumivu makali ya uchungu, jambo ambalo wameonya kuwa ni hatari kwa usalama wa afya zao.

Akizungumzia hali hiyo, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na ujauzito kutoka kitengo cha mama na mtoto Wizara ya Afya, Mzee Nassoro anasema kumekuwa na ongezeko la wanawake wanaotaka kujifungua kwa upasuaji bila kuwepo sababu za kitaalamu.


“Mjamzito anafika hospitali pengine hata siku ya makadirio ya kujifungua haijafika anataka ajifungue kwa upasuaji,” anasema.

Hata hivyo, anasema sababu ya kupoteza muonekano wa maumbile yao ya sehemu za siri haipo, kwani sehemu hiyo imetengenezwa kuwa na uwezo wa kupitisha mtoto kisha kurudi katika hali yake ya kawaida baada ya kujifungua.

Sababu za kitaalamu

Dk Mzee anataja sababu za kitaalamu zinazochangia mwanamke kujifungua kwa upasuaji ni kuokoa maisha ya mama au mtoto na wakati mwingine wote kwa pamoja.


Pia anasema sababu nyingine ya kitaalamu ni endapo mjamzito nyonga yake ni ndogo na kushindwa kupitisha mtoto au mtoto kuwa mkubwa kuliko nyonga ya mama.

Sababu nyingine ni mama kuumwa uchungu kwa muda mrefu, hali hii itachangia kuhatarisha maisha ya mtoto kutokana na kuchoka, hivyo kutakiwa kufanyiwa upasuaji haraka.

Mtaalamu huyo anasema sababu nyingine ni kutangulia kwa kondo la nyuma na kuwepo kwa kizuizi kwenye njia ya uke kutokana na sababu za maradhi, ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi.

Aidha anasema ikiwa mjamzito atapata kifafa cha mimba, madaktari watalazimika kumfanyia upasuaji kabla ya kuumwa uchungu kuepuka madhara wakati wa kujifungua.


“Ujauzito uliopita unaweza kusababisha mama kufanyiwa upasuaji tena kwenye ujauzito ujao kama sababu zilizotokea katika ujauzito uliopita zitajitokeza tena,” anasema.

Kwa upande wa kuokoa maisha ya mtoto, Dk Mzee anasema sababu zinazopaswa kuzingatiwa ni mtoto kuchoka sana, kuwa katika mlalo usio wa kawaida au mtoto kuwa mkubwa kupita kiasi.

Athari upasuaji wa kujitakia

Dk Mzee anasema wakati wa upasuaji kuna hatari kubwa ya mgonjwa kupata madhara ya kiafya au kupoteza maisha.

“Kama mama hana sababu ya kufanyiwa upasuaji kwa nini aingie katika matatizo au kujiweka kwenye hatari zinazotokana na upasuaji?” anahoji Dk Mzee.


Anashauri kujifungua kwa njia ya kawaida kuwa ni bora zaidi kuliko kwa upasuaji, kwani kuna asilimia 70 ya kuhatarisha maisha.

Miongoni mwa athari hizo, Dk Mzee anazitaja kuwa ni dawa ya ganzi kusambaa na kusababisha kifo, uwezekano wa kupoteza maisha kutokana na ajali za upasuaji zinazochangia kuvuja damu nyingi.

Pia upasuaji wakati wa kujifungua husababisha maradhi au uwezekano wa kupata majeraha kwenye kibofu au mirija ya mkojo na kutokea kwa ugonjwa wa fistula.

Hoja hizo zinaungwa mkono na Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na ujauzito kutoka Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Emmanuel Ngadaya anayesema kuomba kujifungua kwa upasuaji kunamsababishia mwanamke kuweka ukomo wa kupata watoto.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, kujifungua kwa njia ya upasuaji huweka ukomo kwa watoto watatu au wanne au kusababisha kujifungua tena kwa upasuaji kwenye ujauzito ujao.


“Hiyo inaweza ikawa sababu ya ukomo wa uzazi kwa mwanamke, kwani kitaalamu tunashauri upasuaji kufanyika kwa mara tatu au isizidi nne kama ikiwezekana.

Dk Ngadaya anasema mwanamke aliyefanyiwa upasuaji ana hatari ya kupasuka kizazi wakati wa kujifungua kutokana na kovu alilopata kwenye upasuaji uliopita na pia kuna hatari kubwa kwa mwanamke huyo kupoteza maisha ikiwa atapata ujauzito mwingine.

Rais wa chama cha madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na wajawazito, Matilda Ngarina anakiri kuwa suala hilo lipo.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad