WATUMISHI wawili wa Shirika la Umeme (TANESCO) wilayani Kahama wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani hapa kwa tuhuma za kuhujumu shirika hilo kwa kuiba mita mbovu na kuwafungia wateja mbalimbali na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh. milioni 10.
Fundi wa TANESCO, akikagua mita ya umeme kwa mteja ili kuwabaini waliounganishia huduma kinyemela kwa kutumia mafundi vishoka kupitia huduma bila malipo katika Kata ya Isagehe, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga jana. Kulia ni moja ya mita mbovu iliyoibwa katika shirika hilo, na kukutwa ikiwa imefungwa katika Kanisa la Kalval Assembel of God (ACG), huku nyaya zinazoruhusu mita kusoma zikiwa hazijaunganishwa na kuruhusu umeme kuingia moja kwa moja kwa mteja. PICHA: SHABAN NJIA
Imedaiwa kuwa vitendo hivyo walikuwa wakivifanya kwa kushirikiana na mafundi vishoka ambao awali walikuwa wakifanya kazi ya kujitolea katika shirika hilo katika miradi mbalimbali ikiwamo ile ya upelekaji wa umeme maeneo ya vijijini.
Kaimu Meneja wa Shirika hilo, Tumain Chonya alibainisha hayo jana alipozungumza na vyombo vya habari, akisema kuwa kati ya Septemba 25 na 29 mwaka huu, walifanya operesheni ya ukaguzi wa mita za wateja wao na kubaini wengi wanatumia huduma kwa muda mrefu bila shirika kufahamu.
Alisema kuwa katika operesheni hiyo walikamata wateja 13 akiwamo kiongozi wa dini na wakazi wengine wanaopata huduma hiyo kwa njia ya undanganyifu, pia wakibaini mmoja wa watumishi wa shirika hilo alipatiwa Sh. 600,000 kinyume cha sheria ili kuwapa huduma ya umeme.
Chonya alisema watumishi hao kwa kushirikiana na mafundi vishoka walikuwa wakiiba vifaa mbalimbali vya TANESCO ndani ya stoo ya shirika na kwenda kuwafungia wateja na kujipatia fedha.
Meneja huyo alitaja baadhi ya vifaa vya umeme vilivyoibwa na kufungiwa wateja hao kuwa ni nyaya za shaba za mifumo ya ardhi inayofungwa kutoka kwenye transfoma hadi ardhini, mita mbovu, nyaya mbalimbali, kobe, mikanda ya kupandia nguzo za umeme na glovu, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. milioni 10.
Alisema mpaka sasa jumla ya transfoma 73 zimehujumiwa kwa kukatwa nyanya za shaba na kuhatarisha usalama wa miundombinu hiyo hasa wakati wa mvua za masika na zaida ya nyaya hizo 1,460 zimeondolewa na kuliingizia hasara shirika kuzirejesha.
"Nimesikitika sana kuona watumishi wangu wanakuwa sehemu ya watu wasiokuwa na uadilifu kuhujumu miundombinu ya shirika, polisi wanaendelea na upelelezi wao na pale watakapokamilisha watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili," alisema.
Chonya aliwataka wananchi wote kutoa taarifa kwa TANESCO na Jeshi la Polisi wanapoona tangu wamefungiwa huduma hajawahi kulipia huduma kwa kuwa wakikamatwa, watashtakiwa kwa jinai ya uhujumu uchumi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi alithibitisha kukamatwa kwa watumishi hao ambao hakutaka kuwataja majina yao ili kutoharibu upelelezi.
Alisema kuwa katika operesheni hiyo walikamatwa watuhumiwa 13. Kati yao, mafundi vishoka ni wanne, watumishi wa shirika hilo wawili na wateja saba waliounganishiwa huduma kwa njia ya udanganyifu na wote watafikishwa mahakamani wakati wowote.