BARAZA la Wauguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), limewafutia leseni wauguzi wasaidizi wawili wa Hospitali ya Wilaya ya Mkomaindo, Masasi mkoani Mtwara, baada ya kupatikana na hatia ya uzembe uliosababisha kifo cha majamzito na mtoto wake.
Wauguzi hao Elizabeth Njenga na Pascal Mnyalu, walishtakiwa kwenye baraza hilo pamoja na wauguzi wengine watatu na madaktari wawili, wote wa hospitali hiyo kuhusika na uzembe uliopoteza maisha ya mjamzito Aisha Romanus.
Wauguzi wengine waliofikishwa katika baraza hilo ni Joyce Nkane na Tumaini Milanzi ambao walipewa onyo kali na Lucia Liababa, ambaye alifutiwa shtaka lake baada ya kuonekana kutohusika moja kwa moja.
Kabla ya hukumu hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Lilian Msele, pia aliwatia hatiani madaktari wawili wa hospitali hiyo, Amina Mushi na Hashimu Chiwaya, ambao taarifa zao zitapelekwa kwenye Baraza la Madaktari ili hatua stahiki zichukuliwe.
Awali dada wa marehemu Agnes John, alilieleza Baraza hilo kuwa Novemba mosi, mwaka jana, mdogo wake Aisha, alishikwa na uchungu wa uzazi na kuamua kumfikisha zahanati ya Lukuledi na muuguzi wa zahanati hiyo baada ya kumpima aliwaeleza waende hospitali ya Wilaya ya Mkomaindo.
Alisema, hata hivyo alipopiga simu hospitali hiyo ya wilaya wauguzi walimjibu hawakuwa na mafuta ya kutumia kwenye gari la wagonjwa na kulazimika kukodi bajaji ambayo pia iliharibika njiani na baada ya matengenezo walifika saa moja usiku hospitali ya Mkomaindo.
Agnes alisema baada ya kupokewa mgonjwa wake hakupata huduma haraka na kuambiwa aondoke jambo alilolipinga na muda mfupi alimuona mdogo wake akiomba msaada kwa wauguzi hao, lakini hawakumjali na ilipofika usiku wa saa tano akaaga dunia.
Wajumbe wa baraza hilo ambao waliwahoji madaktari na wauguzi hao walishangaa baada ya maelezo yao kuwa tofauti kiasi cha mjumbe Haruna Neke kukerwa kutokana na maelezo waliyoyawasilisha awali baada ya kutakiwa kuandika taarifa kutofautiana na maelezo waliyokuwa wakiyatoa.
Kutokana na hukumu hiyo Mwenyekiti wa baraza hilo, Lilian Msele, alisema wauguzi hao hawatotakiwa kufanya shughuli zozote za kiuguzi kutokana na kukiuka kanuni na viapo vyao walivyokula, pia alilaumu uongozi wa hospitali hiyo kutokuawa na ufuatiliaji wa watumishi wake na iwapo usimamizi ungekuwa mzuri maafa kama hayo yasingeweza kutokea.
Naye Msajili wa Baraza hilo, Agnes Mtawa, aliwataka wananchi kufikisha malalamiko yao waonapo hawatendewi haki na wauguzi na madaktari ili wachukue hatua stahiki huku akibainisha kuanza kusikiliza kesi nyingine iliyotoka mkoani Arusha.