Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) limeiagiza timu ya Yanga kumlipa aliyekuwa kocha wao, Luc Eymael dola za kimarekani 152,000 (Sh 354 milioni) kama fidia baada ya kuvunjwa kwa mkataba wake.
Yanga ilimvunjia mkataba kocha huyo Julai 27, 2020 baada ya kutoa maneno ya kibaguzi kwa mashabiki wa klabu hiyo.
Taarifa ya FIFA ilieleza Yanga imepewa siku 45 kuzilipa fedha hizo na wasipofanya ndani ya muda huo watafungiwa kusajili kwenye madirisha matatu.
Alipotatafutwa kocha huyo kuzungumzia kushinda kesi hiyo amesema; ”Taarifa ya FIFA imeeleza kila kitu sina haja ya kuongeza lolote ila ni kweli ipo hivyo.”
Awali Yanga wao walipokuwa wanaachana na kocha huyo walitoa taarifa ikieleza ; ”Klabu ya Yanga inawaomba radhi viongozi wa nchi, Shirikisho la Soka Tanzania, wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga kutokana na kauli za kuudhi na kudhalilisha zilizotolewa na Eymael”.
Kocha huyo wakati anatimuliwa aliiacha Yanga ikiwa nafasi ya pili na kuifanya ishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.