KOCHA Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema uongozi wa klabu hiyo upo makini kusimamia usalama wa timu hiyo na hujuma ambazo wanaweza kufanyiwa Sudan kwa lengo la kuwatoa mchezoni wachezaji.
Yanga inaondoka Oktoba 14 kwenda Sudan kwa ajili ya mchezo wa marudiano kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal utakaochezwa Oktoba 16.
Akizungumza na Spotileo, kocha huyo amekiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu lakini wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatimiza lengo la kucheza hatua ya makundi.
“Kazi yetu kubwa ni kuiandaa timu na siyo kusikiliza maneno ya watu kwamba uwanja wa Al Hilal hatoki mtu. Wao walipata bao hapa kwetu hata sisi tunaweza kupata kwa hiyo mashabiki wetu waondoe hofu,” amesema Kaze.
Yanga inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili kusonga mbele hatua ya makundi.