WAKATI taarifa zikidai mabosi wa Yanga wanafikiria kufumua benchi lao la ufundi chini ya kocha Nasreddine Nabi, Za Ndaani Kabisa zinasema wenzao Azam FC wanasikilizia maamuzi hayo, ili wambebe Mtunisia huyo.
Habari za Ndaani Kabisa zinasema kumetokea mgawanyiko ndani ya uongozi wa Yanga wakipinga juu ya hatua ya kuondoshwa kwa kocha wao Nabi ambaye amekalia kuti kavu ikiwa ni siku chache baada ya timu yao kuondolewa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, mpango huo umekumbana na upinzani mkubwa baada ya vigogo wengine kupinga uamuzi huo.
Upande mwingine mashabiki wa Yanga wanaomnyesha kutokukubaliana na uamuzi huo wakiona bado Nabi bado anafaa kuendelea kuwa kocha wao baada ya kusikia taarifa hizo.
Wakati Yanga hali ikiwa hivyo wenzao Azam wanasubiria maamuzi hayo wakimvizia Nabi ili akachukue mikoba ya Mfaransa Denis Lavagne ambaye tayari wameachana naye.
Azam hawajakubaliana na Lavagne hasa baada ya timu yao kutupwa nje ya Kombe la Shirikisho kisha kupoteza tena mchezo wa tatu wa Ligi dhidi ya KMC wiki hii.
Matajiri hao wa Chamazi wanasubiri maamuzi hayo kama ilivyo Simba kuvizia huduma ya Nabi kuja kufundisha moja ya timu hizo.