JINA la Kiongozi wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, limetajwa katika kesi iliyofunguliwa na wabunge viti maalum 19, katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, kupinga kuvuliwa uanachama wa Chadema.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Jina Hilo limetajwa Leo Alhamisi, tarehe 13 Oktoba 2022 na Wakili wa mjibu maombi namba moja katika kesi hiyo, Peter Kibatala, wakati anamhoji maswali ya dodoso Mbunge Viti Maalum, Hawa Mwaifunga, mahakakani hapo mbele ya Jaji Cyprian Mkeha.
Kesi hiyo namba 26/2022, imefunguliwa na wabunge hao viti maalum wakiongozwa na Halima Mdee, kuiomba mahakama hiyo ifanye mapitio ya kimahakama dhidi ya mchakato uliotumiwa na Chadema kuwavua uanachama, wakidai hakuwa halali kwani hawakupewa nafasi ya kusikilizwa na ulikuwa wa upendeleo.
Katika mahojiano hayo, Wakili Kibatala alimuuliza Mwaifunga kama anamfahamu au hafahamu kuwa Kamati Kuu ya Chadema ilimjadili na kumchukilia hatua Zitto, bila yeye kuwepo kikaoni, ambapo alijibu akidai hakumbuki.
Wakili Kibatala alimuuliza swali Hilo, baada ya Mwaifunga kudai mahakamani hapo kuwa, alifukuzwa Chadema kinyume Cha sheria kwa kuwa hakupewa haki ya kusikilizwa kwani hakushiriki kikao Cha Kamati Kuu Cha chama hicho kilixhofanyika tarehe 27 Novemba 2020, na kutoa adhabu hiyo.
Mahojiano Yao yalikuwa kama ifuatavyi;
Kibatala: Unamfahamu Zitto?
Shahidi: Namfahamu, kiongozi wa ACT-Wazalendo
Kibatala: Unakumbuka ama hukumbuki kwamba Kamati Kuu ilimjadili na kumchukulia hatua bila ya kuwepo?
Shahidi: Mheshimiwa Jaji sikumbuki
Kibatala: Unafahamu Kwa mujibu wa katiba ya Chadema Kamati Kuu Ina mamlaka ya kuchukua hatua za dharura pale maslahi ya chama yanapokuwa hatarini?
Shahidi: Ndio
Zitto alivuliwa uanachama wa Chadema na Kamati Kuu ya chama hicho, mwaka 2011 Kwa tuhuma za kukiuka maadili.
Kesi hiyo imeahirishwa Hadi tarehe 21 Oktoba, 2022, ambapo Mwaifunga ataendelea kuulizwa maswali ya dodoso kuhusu hati ya kiapo alichowasilisha mahakamani hapo, kupinga kufukuzwa Chadema.