NYOTA na nahodha wa Simba, John Bocco imeng’aa kwenye mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting baada ya kufunga mabao matatu ‘hat-trick’ katika ushindi wa 4-0.
Hii inakuwa ni hat-trick ya kwanza kwenye kikosi cha Simba huku ikiwa ni ya pili kwenye ligi baada ya Fiston Mayele wa Yanga kufunga kwenye mchezo wao dhidi ya Singida BS.
Bocco ni mara yake ya kwanza kuanza msimu huu na ametumia dakika 76 kufunga mabao matatu dakika ya 4, 18 na 69.
Nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ anafikisha assisti ya nne msimu huu akitoa pasi ya bao kwa Bocco.
Dakika ya 17 Simba ilishinda bao la pili lililofungwa na Bocco baada ya kugongwa pasi nyingi ndani ya boksi na Clatous Chama alimpigia pasi Bocco aliyefyatua shuti lililojaa kwenye nyavu za Ruvu.
Dakika ya 35 Salum Kipaga wa Ruvu Shooting alimfanyia madhambi Sadio Kanoute wa Simba na kuumia kisha nafasi hiyo akiingia Victor Akpan.
Wachezaji wa Simba wakishangilia bao alilofunga Shomari Kapombe katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting uliochezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa. Picha| Loveness Bernard
Dakika hiyo hiyo Simba ilipata bao baada ya Clatous Chama kupiga pasi ndefu iliyokutana na Shomari Kapombe ambaye alipiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Kiungo mshambuliaji Clatous Chama katika mchezo huo ametoa pasi mbili zilizozaa mabao huku akifikisha assisti tatu kwenye ligi.
Dakika 43 Ruvu Shooting ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Tariq Abeid na Abalkassim Suleiman na kuingia Michael Aidan na Sadat Mohamed.
Simba ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Henock Inonga, John Bocco, Joash Onyango kisha kuingia Mohamed Ouattara, Kibu Denis na Kennedy Juma.
Ushindi huo unaifanya Simba ikae kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 27 ikicheza mechi 12 huku Yanga ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 26 kwenye mechi 10.