Akiri kumuua kaka yake akidai alitaka kumlawiti



MKAZI wa Majohe, Dar es Salaam, Ramadhani Juma, amekiri kumuua kaka yake Fikiri Juma bila kukusudia baada ya kutokea ugomvi baina yao, mshtakiwa huyo akidai chanzo cha ugomvi ni kaka yake huyo kutaka kumlawiti.

Inadaiwa wakati ugomvi huo unaendelea, mshatakiwa alichukua chepe na kumpiga nalo kaka yake kichwani kabla ya kumchoma kisu tumboni, hivyo kusababisha kifo chake.

Ramadhani alikiri kosa hilo la mauaji mwishoni mwa wiki mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Susan Kihawa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kusomewa maelezo ya awali na Wakili wa Serikali, Esther Chale na kuyakubali yote.

Wakili Esther alidai Ramadhani na Fikiri ni ndugu waliokuwa wanaishi pamoja eneo la Majohe jijini Dar es Salaam na kabla ya tukio, mshtakiwa na kaka yake huyo walikuwa na ugomvi, Ramadhani akilalamika kwamba kaka yake Fikiri alitaka kumlawiti.

Alidai ndugu hao walishauriwa na mtu ambaye alitambulika kwa jina la Abdallah Seleman kuwa wanatakiwa kutengena, wasiishi pamoja tena na wote wakakubaliana na ushauri huo wa kutengana.


Hata hivyo, ilidaiwa mahakamani huko kwamba Januari 22, 2017, wakiwa nyumbani, ugomvi uliibuka tena, Fikiri (marehemu) alikuwa akimlalamikia mshtakiwa kwanini amemsaliti.

"Wakati ugomvi huo unaendelea, mshtakiwa alimchukua chepe na kumpiga nalo marehemu kichwani kabla ya kumchoma kisu tumboni na baada ya hapo kilichotokea aliyepigwa alifariki dunia.

"Mshitakiwa alifungua mlango na kuanza kukimbia lakini alikamatwa na polisi jamii na kurudishwa eneo la tukio na wakati wanaingia ndani, walikuta mwili wa marehemu, kisu na chepe vikiwa na damu," alidai Wakili Esther.


Baada ya mshtakiwa kukiri kufanya mauaji hayo, Hakimu Kihawa alimwambia mahakama inaona ana hatia katika kosa la kuua bila kukusudia, huku Wakili Esther akidai hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya mshtakiwa.

Wakili huyo aliomba mahakama itoe adhabu stahiki ili iwe funzo kwa mshtakiwa na kwa watu wengine kwa sababu kitendo kilichofanyika ni cha kukatisha uhai wa mtu.

Baada ya wakili huyo kuwasilisha ombi hilo, Wakili wa Mshtakiwa, Precious Hassan aliomba mteja wake aachiwe kwa masharti kwa sababu akiwa gerezani alilazwa hospitalini kutokana na maradhi ya figo zake kushindwa kufanya kazi na taarifa hizo Jeshi la Magereza linazo.

Pia alidai kuwa kwa miaka mitano na miezi 11, mshtakiwa alipokuwa mahabusu, alipata tatizo la afya ya akili na alipelekewa Hospitali ya Taifa Muhimbili na baadaye alipelekewa Dodoma kwa matibabu zaidi.


Hakimu Kihawa baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, alisema adhabu ya mshtakiwa ataitoa Novemba 29, mwaka huu, huku akiagiza kuwa siku hiyo Jeshi la Magereza liwasilishe mahakamani huko vielelezo vya mshtakiwa kuwa alikuwa mgonjwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad