Novemba 22, 1963 Rais wa 35 wa Marekani, John Kennedy “JFK”, alipigwa risasi na kuuawa. Mshituko ulikuwa mkubwa kuanzia eneo la tukio, Dealey Plaza, Dallas, Texas mpaka Marekani yote.
Ilikuwa Ijumaa. Saa 6:30 adhuhuri kwa Marekani. Mwanaharakati Malcolm X alikuwa msikitini kwa sala ya Ijumaa. Habari za Kennedy kuuawa zilisambaa haraka, kuanzia nyumba za ibada mpaka kumbi za starehe zilizokuwa kwenye pilika za anasa. Mwisho wa wiki uliwadia.
Kiongozi wa Taifa la Kiislamu (NOI), Elijah Muhammad, alitoa tamko kwa wafuasi wake kutotoa maoni kuhusu kifo cha JFK. Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa mwanaharakati Malcolm X. Alishindwa kunyamaza. Alimkaidi kiongozi wake.
Siku hiyo, baada ya kutoka msikitini, Malcom X alipofuatwa na waandishi wa habari ili aeleze mapokeo yake juu ya kifo cha JFK, alijibu: “Being an old farm boy myself, chickens coming home to roost never did make me sad, they always made me glad.”
Tafsiri ya Kiswahili: Kuwa kijana wa shamba wa zamani, binafsi kuona kuku wakirejea kwenye banda kamwe haijawahi kunifanya niwe na majonzi, daima hunipa furaha.
“Chicken come home to roost” ni methali ya Kiingereza ambayo imekuwa ikitumika kwa zaidi ya karne saba sasa. Maana yake ni kuwa ubaya ukishatendwa hurejea kwa aliyeutenda.
Ubaya unafanishwa na kuku wanapotoka bandani, huzunguka kuchakura wakisaka chakula. Hata hivyo, mwisho wa siku, kuku hurejea bandani kulala. Hiyo ni kanuni wa ufugaji wa kuku wa kienyeji.
X alimaanisha kuwa Wazungu wa Marekani walikuwa chanzo cha ubaya duniani, kutesa watu weusi na Wahindi wekundu. Kuvamia mataifa mengine na kusababisha maafa, ulemavu na kadhia nyingine. Hawakujali.
Sasa, ubaya wa Wazungu wa Marekani ulirejea nyumbani, Rais Mzungu, katika taifa ambalo Wazungu wanawakandamiza weusi na Wahindi wekundu, aliuawa. X akasema yeye kama kijana wa shamba wa zamani hakuchukia kuona kuku wakirejea bandani. Maana, ndiyo kawaida.
Bashiru Ally
Unaweza kujitenga na maneno ya X kuwa hakuumizwa na kifo cha JFK, nakushauri uchukue tafsiri ya kuku kurejea bandani, kisha tummulike aliyekuwa Katibu Mkuu CCM, Dk Bashiru Ally. Bashiru pia alipata kuishika ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, kwa muda mfupi mno.
Hivi karibuni, video inayomwonesha Bashiru akihutubia jumuiya ya wakulima wadogo (Mviwata), ilisambaa kwa kasi. Bashiru alikuwa akiwaeleza wakulima umuhimu wao kwa mustakabali wa nchi.
Utaona kuwa hoja ya Bashiru ilikuwa nzuri mpaka pale alipoanza kutoa matamshi ya kukwazwa na sifa anazopewa Rais Samia Suluhu Hassan. Kwamba kuna mawakala humdanganya kwamba anaupiga mwingi.
Bashiru hakutaja jina la Samia. Hata hivyo, maneno “anaupiga mwingi”, yalipata umaarufu mno pale watu walipokuwa wakiuelezea utendaji wa Rais Samia, kwamba anafanya kazi nzuri. Wakitumia lugha ya soka kuwa anaupiga mwingi.
Katika hoja yake, Bashiru aliitaka jumuiya ya wakulima wadogo kutopenda kutoa shukurani kwa Serikali na kumsifu Rais Samia kwamba anaupiga mwingi. Kwamba wakifanya hivyo, watapoteza maana.
Mpaka hapo ukichukua maneno peke yake, huoni kama Bashiru alizungumza vibaya. Aliwakumbusha wakulima umuhimu wao, vilevile haki na wajibu ambao wanapaswa kuujenga mbele ya watu aliowaita wanyonyaji na watawala.
Dhambi ya Bashiru
Tukope maneno yaliyotamkwa Siku ya 74 ya kalenda ya Roma (Ides of March). Mwaka ulikuwa wa 44 Kabla ya Kristo (BC). Siku hiyo alikuwa anauawa mtawala wa zamani wa Roma, Julius Caesar.
Caesar hakutegemea kama kijana wake, Marcus Brutus, aliyepata kumsaliti kisha akamsamehe, angeweza kumgeuka tena kuwa mstari wa mbele katika mpango wa kukatisha uhai wake. Caesar alipomwona Brutus, alimuuliza kwa Kilatini: “Et tu, Brutus?” – “Hata wewe, Brutus?”
Nakopa maneno hayo ya Caesar “Hata wewe, Brutus?” kisha nayageuza kidogo kumwelekea Bashiru: “Hata wewe, Bashiru?” Swali kwa Bashiru si kwa tafsiri ya usaliti wa kuua kama Brutus kwa Caesar, bali kwa kusahau haraka. Wote wasahau, hata Bashiru jamani?
Miaka imepita ila kumbukumbu za matukio zinafanya ionekane kama juzi tu. Bashiru akiwa Katibu Mkuu CCM. Likaibuka kundi la watu walioamua kumsifia aliyekuwa Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli.
Wabunge wa upinzani walihama vyama vyao na kuisababishia nchi hasara ya kurudia uchaguzi. Waliohama walisema “wanaunga mkono juhudi za Rais Magufuli”, naye Bashiru aliwapokea. Akawakumbatia.
Watu walewale waliojiuzulu ubunge na kuhama vyama, Bashiru akiwa Mwenyekiti wa Sekretarieti ya CCM, alihakikisha hakuna mchakato wa ndani ili wasishindane na wana-CCM wengine katika kupata tiketi ya kugombea ubunge jimbo lililokuwa wazi.
Waliohamia CCM walisimamishwa kugombea ubunge kwenye majimbo waliyojiuzulu na kushinda tena. Yapo maeneo nguvu iliyotumika ilikuwa kubwa mpaka damu ilimwagika. Aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, alipigwa risasi katika vurugu za uchaguzi wa marudio Kinondoni.
Aliyekuwa mbunge wa Kinondoni kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maulid Mtulia, alijiuzulu kwa usemi kuwa “aliunga mkono juhudi za Rais Magufuli kuleta maendeleo”. Bashiru alikuwa hajawa Katibu Mkuu, aliona. Kisha akakubali uteuzi.
Baada ya Bashiru kuwa Katibu Mkuu, kasi ya wabunge na madiwani wapinzani kuachia viti vyao na kuiiunga CCM ilikuwa kubwa. Bashiru alisimamia michakato yote na alikwenda kuwafanyia kampeni waliohamia CCM.
Ni kipindi ambacho kumsifia Dk Magufuli kwa mapambio ya kila aina ilionekana ndio ‘fasheni’ na Bashiru hakukerwa. Kuna kipindi mapambio ya Magufuli yalivuka kiwango cha sifa za kawaida za binadamu, lakini Bashiru hakuchukizwa.
Yaliibuka magazeti yenye kushambulia watu na kuwapa uhusika mbaya, vilevile yakawa yanamsifu Magufuli. Magazeti yalikosa weledi na kuchafua hadhi ya taaluma ya habari. Bashiru hakuwahi kukasirishwa.
Mwandishi wa habari, Cyprian Musiba, aliibuka kinara wa kumsifu Magufuli na kushambulia watu aliodai wanataka kumhujumu Rais huyo wa tano wa Tanzania.
Waliotajwa na Musiba walipata mitikisiko mikubwa. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe alipitishwa kwenye bomba la moto mpaka akafukuzwa uanachama.
Aliyekuwa Katibu Mkuu CCM, Kanali mstaafu, Abdulrahman Kinana alifungiwa kugombea nafasi yoyote ya uongozi. Yusuf Makamba ambaye naye alishakalia kiti cha Katibu Mkuu CCM, ilibidi aombe radhi yaishe.
Kisa, walitajwa na Musiba kuwa walikuwa wanamhujumu Magufuli. Bashiru hakuwahi hata kutoa tamko la kumwonya Musiba, au kumwita na kuketi pamoja na aliowatuhumu ili kupata mwafaka au kujua kiini na ukweli.
Leo Bashiru anachukia watu kusema “Rais Samia anaupiga mwingi”, kipindi cha Magufuli, wabunge walitia fora. Angesimama mbunge na kutumia zaidi ya nusu ya muda aliopewa kuchangia bungeni, kumsifu Magufuli.
Aliitwa “Chuma”, “Jembe”, “Rais wa Wanyonge”, “Kiboko ya Wapinzani”, “Kiboko ya Mabeberu”, “Kiongozi wa Malaika”, na majina mengi ya mapambio, hakuna mahali Bashiru alichukia.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, alipata kusema (na video zipo), kwamba kwa kazi nzuri aliyoifanya, watu wa Tabora watamwambia Mungu amshukuru Magufuli. Bashiru hakuogopa hata hii kauli kuwa Muumba ndiye ampe shukurani muumbwa, Magufuli.
Kuku wanarudi bandani
Kuitendea haki kauli ya Bashiru lazima kuigawa katika pande nne. La kwanza ni kuwa tabia ya kusifu sana viongozi sio nzuri. Inalemaza. Huwapa viongozi u-Mungu mtu. Ndivyo akina Bashiru walimtengeneza Magufuli.
Alichokisema Bashiru ni sahihi, lakini katika kinywa ambacho hakina usahihi. Tunahitaji kuona nchi ina viongozi wanaowajibika ipasavyo kwa wananchi na sio kubeba tafsiri kuwa wanachokifanya ni msaada. Bashiru ni sehemu ya walioleta hayo mazingira ya kubadili utumishi wa viongozi kuwa msaada.
Pili, ni ukumbusho kwa viongozi walio kwenye nafasi leo. Wasiwe chawa wa mabosi wao, bali waitende kazi inavyotakiwa. Wanapaswa kumshauri jinsi ya kupokea sifa na kutenda. Kiongozi lazima awe mnyenyekevu kwa wananchi.
Bashiru hakuifanya kazi yake vizuri kipindi cha Magufuli, kumshauri namna bora ya kuishi kama Rais na kutolemazwa na sifa mfululizo. Alifurahia cheo kutoka Katibu Mkuu CCM mpaka Katibu Mkuu Kiongozi.
Hivi sasa yupo nje ya cheo ndio anakumbuka kuwa sifa nyingi kwa viongozi sio sawa. Hii ina maana iwasaidie na walio kwenye mfumo leo, si sawa sana kumsifu Rais Samia mpaka kupitiliza. Wamshauri na wampongeze anapostahili. Sio sifa kedekede mpaka zimlemaze.
Viongozi wote ni binadamu. Hawana sifa ya malaika. Wanapatia na wanakosea. Sifa zikiwa nyingi, kiongozi anaweza kudhani kila kitu kipo sawa. Haya ni madhara makubwa.
Tatu, Bashiru ni mbunge wa kuteuliwa. Anayo nafasi ya kuwasaidia wakulima kwa kujenga hoja bungeni, ama kwa maneno au maandishi. Mbunge hupaswa kubeba shida za wananchi na kwenda kuzisemea.
Haipaswi mbunge kwenda kuwachochea wananchi dhidi ya Serikali, wakati yeye ndiye mwakilishi wao. Haya Bashiru anayajua. Ni mwanzuoni, anajua jinsi mhimili wa uwakilishi (Bunge), unavyopaswa kufanya kazi na Serikali. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Bashiru anachukuliwa ana nongwa na sifa za Rais Samia.
Nne, tangu Bashiru alipotoa maoni yake, chama chake kinamshughulikia kwelikweli. Vijana hawakumbuki kama alipata kuwa Katibu Mkuu wao. Haya ndio matokeo halisi ya kuku kurejea bandani.
Bashiru alipokuwa Katibu Mkuu CCM, vijana wa chama hawakuwa na adabu kwa wastaafu. Musiba, Ally Hapi, Livingstone Lusinde, Hussein Bashe, hawakuwa na adabu kwa akina Makamba na Kinana. Wazee walishughulikiwa, naye alinyamaza.
Ona leo, Lusinde anamshughulikia Bashiru. Katibu wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Kenani Kihongosi, anampa maneno makavu bila staha kuwa alikuwa kiongozi wao mwandamizi. Ni malipo. Kuku ambao Bashiru aliwafuga, wanarejea bandani.
Source: Mwananchi