Aliyefungwa kwa kubaka, kuambukiza Ukimwi aachiwa Huru




Shinyanga. Hamimu Yunusu, mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga ambaye mwaka 2018 alihukumiwa kifungo cha miaka 34 jela kwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la nne na kumwambukiza Ukimwi kwa makusudi, ameachiwa huru.

Hukumu ya Yunusu ilijumuisha kifungo cha miaka 30 kwa kubaka na miaka minne kwa kumwambukiza Ukimwi mwanafunzi huyo kwa makusudi. Hata hivyo, Ijumaa ya Novemba 4 mwaka huu, milango ya matumaini ilifunguka kwake baada ya Mahakama ya Rufani kumwachia huru.

Yunusu amerudi uraiani baaba ya jopo la majaji watatu ambao ni Augustine Mwarija, Rehema Kerefu na Panterine Kente kuzikubali hoja za rufaa aliyoiwasilisha kupinga adhabu hiyo baada ya kubaini dosari za kisheria katika uchukuaji ushahidi kutoka kwa mtoto huyo na wenzake.

Hata hivyo, baadhi ya mawakili na watetezi wa haki za binadamu wamekuwa na maoni tofauti juu ya hukumu za kesi za aina hiyo na nyingine kufutwa au kuagiza kusikilizwa upya kutokana na dosari za kisheria za baadhi ya majaji au mahakimu.


Baadhi ya mawakili hao wamesema ni wajibu wa maofisa wa mahakama ambao ni mawakili wa mashitaka na utetezi, kumkumbusha jaji au hakimu pale anapopitiwa katika uchukuaji wa taarifa za mwenendo wa kesi kwa kuwa nao ni binadamu.

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Rwezaura Kaijage anasema dosari katika mwenendo hujirudia kwa kuwa mfumo wa mahakama hauna utaratibu wa kumwajibisha jaji au hakimu anayekwenda kinyume na taaluma yake.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THDRC) umesema ili hukumu iwe sahihi ni lazima ifuate misingi na taratibu za kisheria na ndio maana kuna Mahakama ya Rufani inayoangalia kama adhabu ilitolewa kwa mujibu wa sheria.

Kauli za mawakili hao zimetokana si kwa kuzingatia kesi hiyo ya Shinyanga pekee, bali kuongezeka kwa idadi ya hukumu za ubakaji au ulawiti kwa watoto kufutwa kutokana na dosari katika uchukuaji wa ushahidi wa mtoto.

Sheria inataka kabla ya kuchukuliwa ushahidi, mtoto ale kiapo kinachosema atasema ukweli lakini utaratibu huo haufuatwi na baadhi ya mahakimu na kuzalisha sababu za rufaa.

Dosari nyingine ambayo husababisha kufutwa kwa hukumu za kesi na kuagizwa kusikilizwa upya na jaji mwingine, ni baadhi ya majaji kutowasomea wazee wa mahakama muhtasari wa ushahidi.

Kaijage ambaye ni wakili pia alisema mfumo wa uteuzi wa majaji ni dhaifu kwani hakuna chombo cha kumkataa mtu aliyeteuliwa na Rais hata kama hafai au hana sifa hiyo.


“Hiki ndio chanzo cha hukumu mbaya na wakati mwingine zinazogongana. Hebu Rais atupe siku moja nafasi ya ku-criticize (kukosoa) majaji na mahakimu wanaopewa hizo nafasi uone kivumbi,” alisema Wakili Kaijage.

Kesi ilivyokuwa

Katika kesi hiyo, Yunusu alitiwa hatiani kwa makosa mawili, la kumbaka mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 14 kinyume cha kanuni ya adhabu na kusambaza Virusi vya Ukimwi (HIV) kwa makusudi.

Ushahidi ulieleza kati ya Aprili 2015 na Februari 2018 katika eneo la Mhongo wilayani Kahama, ilidaiwa mshitakiwa alimbaka mtoto huyo na kwa makusudi akamwambukiza Ukimwi.

Katika ushahidi wake, mtoto huyo alieleza kuwa mshitakiwa alikuwa mpenzi wake tangu mwaka 2014 wakati huo akiwa na umri wa miaka 11 na mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mhongolo iliyopo Kahama.

Aliieleza mahakama kuwa siku moja, Aprili 2014 alikuwa akienda kuchota maji mtoni akiwa na baiskeli na akiwa njiani wakati amesimama kurekebisha mnyororo wa baiskeli yake, alitokea mshitakiwa akiwa na pikipiki.

Alipomuoana akirekebisha baiskeli yake, mshitakiwa aliegesha pikipiki na akamkamata na kumpeleka katika nyumba ambayo ujenzi wake haujamalizika (pagale), akamziba mdomo na kumlaza chini kisha kumvua nguo naye akashusha suruali yake na kumbaka.

Alieleza kuwa mshitakiwa alimuonya na kumtisha kuwa asije akasema juu ya jambo hilo kwa mtu yeyote kwani angemuua na alipofika nyumbani hakumwambia mtu kwani lile onyo la mshitakiwa lilikuwa linamsumbua kichwani.

Baada ya siku mbili, kwa mujibu wa ushahidi wake, wakati akienda tena kuchota maji, mshitakiwa alimfuata na kumchukua tena na kumpeleka katika pagale lilelile na kumbaka na baada ya siku hiyo, ikawa ni mchezo wao kufanya hivyo.

Kuna wakati walifanya kitendo hicho nyumbani kwa mtuhumiwa wakati mkewe hayupo na nyakati hizo mshitakiwa alikuwa akimpa Sh1,000 na waliendelea hivyo hadi mwaka 2018 ambapo baba wa mtoto alijulishwa kwa siri juu ya jambo hilo.


Baada ya kuelezwa hivyo, baba alimuuliza mdogo wa binti huyo ambaye alisema ni kweli amekuwa akimuona dada yake akienda mara kwa mara nyumbani kwa mshitakiwa ndipo baba alitoa taarifa polisi na mshitakiwa alikamatwa na wote wawili (mtoto na mshitakiwa) walipelekwa hospitali na vipimo vilithibitisha mtoto kubakwa na wote wawili kubainika wana maambukizi ya Ukimwi.

Katika utetezi wake uliokataliwa na hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, mshitakiwa alikanusha kutenda makosa hayo mawili na kwamba kesi hiyo ilitengenezwa na shahidi wa tatu ambaye alikuwa na mgogoro naye wa ardhi.

Ni kutokana na ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka, mahakama ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 34 jela ambayo hakuridhika nayo hivyo akakata rufaa Mahakama Kuu Shinyanga ambayo ilibariki kuwa alistahili adhabu hiyo.

Rufaa yake

Yunusu hakuridhika na hukumu hiyo hivyo akaamua kuomba kusikilizwa na Mahakama ya Rufani Tanzania akisisitiza hakuwa na hatia akitoa sababu sita ikiwamo upande wa mashitaka kutothibitisha shtaka hilo pasipo kuacha mashaka.

Pia, aklisema hakuna ushahidi ulioletwa kutoka shule aliyokuwa anasoma mtoto, ushahidi ulioletwa na upande wa mashitaka ulikuwa dhaifu na hauaminiki, mahakama haikuzingatia utetezi wake na umri wa mtoto huyo haukuthibitishwa.

Wakati wa kusikilizwa kwa rufaa yake na jopo la majaji hao, Yunusu alijitetea mwenyewe wakati Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili wa Serikali, Mercy Ngowi, Caroline Mushi na Rose Kimaro kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS).

Wakili Ngowi licha ya kupinga rufaa hiyo na kuwasilisha hoja mbalimbali kuunga mkono hukumu, alikiri kuwa ushahidi wa mtoto huyo ulichukuliwa kinyume na takwa la lazima la Kifungu cha 127(2) cha Sheria ya Ushahidi kilichorejewa mwaka 2022.

Kulingana na wakili huyo, kifungu hicho kinataka mtoto aahidi kusema ukweli na sio uongo na kama hakueleza hayo kabla ya kutoa ushahidi wake, hilo linathibitika kupitia Kifungu cha 127(6) cha sheria hiyo.

Wakili huyo alisema maelezo ya mtoto huyo ni ushahidi bora ambao unaweza kutumiwa na mahakama kumtia hatiani mshitakiwa bila hata kuungwa mkono ilmradi mahakama iliridhika kuwa mtoto huyo alikuwa anasema ukweli.

Lakini wakili huyo alikubali hoja kwamba ushahidi wa shahidi wa tano ambaye ni mtoto ulichukuliwa kwa kukiuka sheria hiyo na kuomba uondolewe kwenye kumbukumbu za mahakama akisisitiza kwamba hautoathiri kesi hiyo kwa sababu ushahidi wa mtoto aliyefanyiwa kitendo hicho uliungwa mkono na shahidi wa pili, watatu na wa nne na upande wa mashitaka uliuthibitisha kwa viwango vinavyotakiwa.

Kama mahakama hiyo itaona ushahidi wa mtoto huyo ulichukuliwa na mahakama kwa kukiuka taratibu, alisema itakuwa vyema ikaamuru kesi hiyo isikilizwe upya kwa kuwa dosari hiyo ilifanywa na mahakama hivyo mzigo asibebeshwe mtoto aliyetendwa.

Uamuzi wa majaji

Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, majaji walisema sheria ya ushahidi inasema shahidi yeyote ataapa kwanza kabla ya kutoa ushahidi wake na kwa mtoto anaweza kutoa ushahidi wake pasipo kula kiapo hicho kama inavyotakiwa kwa mtu mzima.

Hata hivyo walisema kwa shahidi mtoto, kifungu hicho cha 127(2) cha sheria namba 4 iliyoanza kutumika Julai 8 mwaka 2016 kinamtaka kabla ya kuanza kutoa ushahidi, aahidi kuwa atasema ukweli mbele ya mahakama.

“Kwa shauri lililopo mbele yetu, hakuna ubishi kuwa wakati anatoa ushahidi alikuwa na umri wa miaka 14. Pia hakuna ubishi kuwa kama alivyokubali kwa usahihi Wakili Ngowi kwamba mahakama haikizingatia kifugu cha 127(2),” walisema jaji.

Majaji hao walisema katika kesi hiyo, Mahakama ya Wilaya ya Kahama ilikosea kisheria kuchukua ushahidi wa mtoto huyo kwa kukiuka takwa la lazima la kisheria hivyo kwa uamuzi mwingine uliotolewa, wanauondoa ushahidi huo.

“Kwa msingi huohuo, na kama alivyosema kwa usahihi Wakili Ngowi kwamba hata ushahidi wa shahidi wa tano nao ulikiuka sheria, nao unastahili kutozingatiwa hivyo unaondolewa kwenye kumbukumbu za mahakama,” walisema majaji hao kwenye uamuzi wao. Baada ya kuuondoa ushahidi wa shahidi wa kwanza (mwathirika) ambao ndio ushahidi bora katika kesi ya makosa ya kujamiiana, majaji hao walisema wanaona ushahidi wa mashahidi wa pili, tatu, nne na sita hauna nguvu kuthibitisha shtaka hili wakitolea mfano ushahidi wa shahidi wa tatu uliegemea kwenye hisia kutokana na shahidi wa kwanza kwenda mara kwa mara kwenye nyumba ya mshitakiwa na ushahidi wa shahidi wa nne na wa sita wote ulikuwa ni wa kuambiwa.

Majaji hao katika uchambuzi wao, walisema hata ushahidi wa shahidi wa shahidi wa pili ambaye ni daktari, ulithibitisha tu kuwa uke wa mtoto uliingiliwa na kwamba ameathirika na Ukimwi lakini hauonyeshi kama ni mshitakiwa ndiye alimwambukiza maradhi hayo mtoto huyo.

Kwa mazingira hayo, majaji hao walisema wanaridhika kuwa hakuna ushahidi uliobaki katika kumbukumbu za mahakama ambao ungeweza kutumiwa na mahakama iliyosikiliza kesi hiyo kuweza kumtia hatiani mshitakiwa.

“Ni maoni yetu zaidi kwamba kama mahakama ya kwanza ya rufaa ingezingatia masuala yaliyojadiliwa hapo juu, ingefikia hatua isiyoweza kuepukika kwamba ilikuwa salama na kuendeleza (kubariki) hukumu kwa mrufani,” walisisitiza majaji hao watatu.

Watetezi wanena

Wakili Peter Mshikilwa wa jijini Dar es Salaam alisema kwa maoni yake, anaona kuna haja ya kuutathmini mhimili wa mahakama na wadau wote wa utoaji haki ili kutomwachia mtu kwa kutumia makosa ya kiufundi ya kisheria.

“Hii kuachia mtu kwa sababu za legal technicalities (makosa ya kiufundi ya kisheria) hata katika ushahidi ulio wazi kunafifisha imani ya taasisi za utoaji haki. Madhara ya huyu mtoto hayawezi kufidiwa katika maisha yake yote,” alisema wakili huyo.

Wakili Elia Kiwia wa mjini Moshi alisema kikubwa kinachotakiwa ni umakini na kuwa na wanasheria wanaopenda kujifunza kwani hata pale ambapo jaji au hakimu anapojisahau, basi wao kama maofisa wa mahamama wamkumbushe.

“Mara nyingi ni overlook (kupitiwa) au wakati mwingine mawakili kutokupitia walipoishia siku ya mwisho na kuendelea. Jambo lingine ni kuacha procedures (taratibu) nyingine zikiwa hazijafanyika na kuendelea na kesi,” alisema Wakili Kiwia.

Wakili Patrick Paul alisema suala la mtoto kutakiwa kuieleza mahakama kuwa atasema ukweli kabla ya kutoa ushahidi ni hitaji muhimu la kisheria kwani anapaswa kufahamu umuhimu wa kusema ukweli.

“Hii ni kwa sababu ushahidi ndio unaomtia mtu hatiani au kumwachia huru na hilo litapatikana kutokana na ushahidi wa kweli. Mwendesha mashitaka ndio anapaswa kuhakikisha utaratibu huu unafuatwa,” alisisitiza Paul.

Mratibu wa THDRC, Onesmo Olengurumwa alisema ili hukumu iwe sahihi ni lazima ifuate misingi na taratibu za kisheria na ndio maana kuna Mahakama ya Rufani kuangalia kama adhabu ilitolewa kwa mujibu wa sheria.

“Ili kutumia ushahidi fulani kuna taratibu zinapaswa kufuatwa ili uweze kutumika hasa ushahidi wa mtoto kuna utaratibu wa kufanya ili uonekane una nguvu. Sasa kama watu wana skip (kuruka) ndio mwisho wa siku inaleta shida,” alisema Olengurumwa.

Changamoto iliyopo Tanzania, alisema ni kukosekana kwa mashirika au watu ambao wana review (kupitia) baadhi ya hukumu na kuzitolea mapendekezo ya nini kifanyike kwani majaji na mahakimu ni binadamu kama wengine ambao huweza hufanya makosa yanayosababisha upande mmoja ukose haki unaostahili.

“Kuna wakati wanahitaji muda wa kujinoa upya, muda wa kukumbushana majukumu yao, muda wa kupitia upya na ukizingatia majaji na mahakimu wengine wanaoingia kwa sasa ni wapya. Ni suala la kukumbushana mara kwa mara,” alisisitiza mttezi huyo wa haki za binadamu.

Ole Ngurumwa alipendekeza kuwe na warsha za kujadili changamoto kama hizo kwani inaweza kusaidia kuziepuka hasa zile ambazo zimekuwa zikijirudia mara kwa mara hivyo kuwanyima haki baadhi ya watu wanaostahili.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad