Baada ya Kutua Tunisia, Kocha Nabi Akuna Kichwa na Kupangua Kikosi Chote


YANGA imeshatua nchini Tunisia tayari kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Club Africain, huku kocha wa timu hiyo Nasreddine Nabi akikikuna kichwa ili kukifumua kikosi hicho katika safu yake ya ulinzi na kiungo.

Msafara wa timu hiyo wenye wachezaji 23, ulitua juzi jijini Tunis kisha kuunganisha usafiri hadi Mji wa Swis ambako itaweka kambi fupi ya siku mbili kabla ya kurejea tena jijini humo kwa mchezo wa play-off wa kuwania kuingia makundi ya Shirikisho Afrika utakaopigwa Jumatano ijayo.

Katika mechi ya kwanza Yanga ililazimishwa suluhu nyumbani na hivyo mechi hiyo ya marudiano itahitajika kushinda au kupata sare yoyote ya mabao ili kurejea rekodi yao ya mwaka 2016 na 2018 ilipotinga makundi ya michuano hiyo baada ya awali kutolewa Ligi ya Mabingwa kama ilivyo msimu huu.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Tunisia, Nabi alisema anatambua mchezo huo utakuwa mgumu na kukosekana kwa beki wa kulia, Mkongomani Djuma Shaban kunamlazimisha kufanya mabadiliko makubwa katika ukuta wake.

Nabi alisema anafikiria kuwandaa mabeki Dickson Job, Joyce Lomalisa, Kibwana Shomari na hata Farid Mussa kuangaliwa kupewa majukumu tofauti katika kikosi chake.

Huenda Nabi akampa Job na Kibwana kucheza kama beki wa kulia huku pia Farid na Lomalisa kucheza kama mabeki wa kushoto.

“Tunatakiwa utulivu mkubwa wa kuzuia, tunahitaji kucheza kwa nidhamu kubwa kwa kuwa hatutaki kuwapa nafasi ya kukamilisha mashambulizi yao, nafahamu wanaweza kuwatumia wachezaji wao mawinga wanaokimbia sana katika mechi hii ya marudiano ambao hawakucheza kule Tanzania,” alisema Nabi na kuongeza;

“Tutaangalia nani anatuonyesha kukamilisha tunachotaka wafanye katika mazoezi yetu, ni hatua nzuri tutakwenda Swis kule tutakuwa na uhuru wa kujiandaa kwa utulivu kuliko kubaki pale Tunis, ule ni mji wa wapinzani wetu.”


Nabi alisema pia anafikiria kupangua safu ya kiungo kuhakikisha wanakuwa na makali ya kusukuma mashambulizi ya haraka katika ukuta wa wapinzani wao.

Kuna uwezekano Nabi akamhamisha kiungo wake Feisal Salum kutoka nafasi ya ukabaji kumpandisha hadi kiungo wa juu mshambuliaji nyuma ya mshambuliaji wa mwisho Fiston Mayele huku Stephan Aziz KI akitokea pembeni.

Mabadiliko ya kumsogeza juu Feisal yanaweza kumrudisha kikosini kiungo fundi wa pasi Salum Abubakar ‘Sure boy’ au Zawadi Mauya mmoja wao kucheza sambamba na Khalid Aucho katika eneo hilo, huku Yanick Bangala na Bakar Mwamnyeto wakasimama kama mabeki wa kati kumlinda kipa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad