Dar es Salaam. Unaweza kusema bado giza nene na inaweza kuchukua muda kujua nini hasa sababu ya kuanguka kwa ndege ya Precision Air iliyopata ajali na kuua watu 19.
Hata hivyo, imefahamika kuwa wachunguzi wa chanzo hicho watalazimika kuwahoji watu watatu wanaohusika kuhakikisha usalama wa ndege kabla na baada ya kuruka ili kupata majibu ya nini hasa kilisababisha ajali hiyo.
Kwa mujibu wa ramani hiyo ya uchunguzi, maelezo yanaweza kutolewa na mtuma ndege (an airplane dispatcher) wa Precision Air aliyekuwa zamu siku hiyo, mhandisi wa ndege (ground engineer) na wa tatu aliyetakiwa rubani wa ndege iliyopata ajali, ambaye hata hivyo, alifariki dunia ajalini.
Ndege ya 5H-PWF, ATR 42-500 yenye uwezo wa kubeba abiria 48 ilianguka Ziwa Victoria karibu na uwanja wa Ndege wa Bukoba Jumapili saa 02:53 asubuhi ikitokea Dar es Salaam kwa kile kinachoelezwa kuwa ni hali mbaya ya hewa.
Ilikuwa na abiria 39 (watu wazima 38 na mtoto mmoja) na wafanyakazi wanne.
Hadi sasa, hali mbaya ya hewa (upepo mkali na mvua) ndivyo vinadaiwa kuizuia ndege hiyo kutua Bukoba na kumfanya rubani wake kutumia muda mwingi angani akitafuta namna ya kutua salama.
Kabla ndege kuruka
Wataalamu wa masuala ya anga na marubani waliozungumza na Mwananchi wamesema kwa mujibu wa utaratibu wa uendeshaji wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), lazima rubani wa ndege ajulishwe kabla ya kupaa, hali ya hewa angani na anakokwenda.
Kwa mujibu wa viwango hivyo vya kimataifa, anayeruhusu ndege atapaswa kwanza kuwajibika endapo ataruhusu ndege iondoke huku kukiwa na hali mbaya ya hewa.
“Mtu huyu lazima apate ripoti ya hali ya hewa kutoka vyanzo muhimu ikiwemo Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na picha za setelaliti, atakosea sana ku-release flight (kuruhusu ndege) kama hali ya hewa si rafiki.
“Kwa hiyo huwezi kuanza kutafuta chanzo cha ajali hii kuanzia Bukoba, si tatizo la Bukoba pekee, yalianzaia hapa Dar es Salaam. Kuna broken chain of command kwenye tatizo hili,” anasema Katibu wa Chama cha Marubani Tanzania, Tanzania (Tapa), Kapteni Khalil Iqbal.
Katika utaratibu wa kawaida, TMA hutoa taarifa kamili ya hali ya hewa (flight weather dispatch folder) kwa mtuma ndege, yenye taarifa ya hali ya hewa ya siku hiyo ikiwemo mwelekeo wa upepo, hali ya mawingu na mvua au radi. Rubani wa ndege pia hushirikishwa kuhusu hali hiyo.
Utaratibu mwingine wa usafiri wa anga ni kwamba ripoti za hali ya hewa zitakazotumika kwa usalama wa ndege hutolewa saa sita kabla ya safari na nyingine saa moja kabla ya safari.
Wachunguzi wa ajali hiyo watalazimika pia kumhoji mdhibiti wa kitengo cha uendeshaji (Operations Control Centre-OCC) ambaye aliwasiliana na rubani tangu ndege ilipotoka Dar es Salaam hadi hatua ya mwisho.
Mtu mwingine ambaye atalazimika kutoa ushahidi kwa wachunguzi ni ofisa uendeshaji wa ndege (flight operations officer) ambaye jukumu lake kubwa ni kufuatilia ndege zote za kampuni yake zilizoko angani na kutoa taarifa.
Ingawa amefariki, mawasiliano ya rubani wa ndege hiyo na waongoza ndege yatatoa mwanga mkubwa wa nini hasa kilimsibu hadi ndege kutua ziwani.
Kwa kawaida, rubani wa ndege pia hushirikishwa taarifa zote za hali ya hewa ili zimsaidie kufanya uamuzi sahihi wa kurusha ndege au la.
Mawasiliano ya rubani na waongoza ndege yanaweza kupatikana kupitia kisanduku cheusi (black box) kinachotunza data za ndege jinsi inavyoendeshwa, kifaa cha kutunzia sauti, cockpit voice recorder, kinachohifadhi sauti kati ya rubani na yeyote anayewasiliana naye.
“Yeye (flight operations director) ndiye wa kwanza kubanwa. Kwa nini ali-release flight (aliruhusu ndege)” anahoji Iqbar.
Marubani tumeachwa
Rubani mwingine aliyeomba kutotajwa jina ameliambia gazeti hili kuwa ajali ya Bukoba ni wito tosha kwa Serikali kusikiliza malalamiko ya muda mrefu ya marubani, akidai kazi yao imegubikwa na changamoto nyingi.
Anadai kwa muda mrefu mamlaka ya anga imepuuza malalamiko na maonyo wanayotoa kuhusu usalama wa ndege, akidai wamewahi kujikuta wakilazimishwa kurusha ndege hata katika mazingira yasiyoruhusu.
“Kuna marubani tuliteswa sana siku za nyuma, ukikataa kurusha ndege kwa sababu genuine (za msingi) kabisa unaambiwa ‘sisi ni shirika la miaka mingi, rusha ndege kwa kuwa watu tayari wako airport na wamekata tiketi.’
“Bahati mbaya ukipeleka ripoti mamlaka ya anga kuwa nimekataa kuruka kwa sababu ya hatari hawakusikilizi, sana sana wataishia kukuchongea kwa wamiliki wa ndege, hivyo wengi hujikuta wanakiuka miiko ya kazi kutokana na operation pressure (msukumo wa kiutendani) inayotokana na maamuzi ya watendaji wakuu. Matatizo ni makubwa katika sekta ya anga.
“Tumempelekea waziri masuala yetu takafikiri atamwita mkurugenzi mkuu wa TCAA lakini hakuna kinachofanyika. Huko kwenye mamlaka kuna matatizo makubwa sana kuanzia suala zima la kupanga na kutekeleza vitu. Wanaungana na wamiliki wa kampuni za ndege kuzima malalamiko yetu,” alidai rubani huyo.
Kwa upande wake, Iqbal alidai kuwa kamati ya usalama wa anga wamekuwa wakipeleka siri za malalamiko yao kwa wamiliki wa ndege na kuziweka ajira zao katika mazingira magumu.
“Kuna rubani alipeleka malalamiko kwenye kampuni yake kuwa ‘siwezi kuruka kwa sababu uwanja anaotakiwa kutua haukuwa na taa’, akafukuzwa kazi.
“Kuna kampuni ndege zao zilikuwa na injini za zamani na zilikuwa zimechoka. Marubani wakapeleka taarifa mamlaka ya anga, rubani akafukuzwa,” alidai.
Viongozi TCAA wamulikwe
Madau mwingine wa anga amedai kuwa ni aibu kwa taasisi nyeti kama Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA) kuongozwa na watu wasio na taaluma ya masuala ya sekta ya anga.
“Hawajui mambo ya anga. Tunapata mashaka makubwa kuwekewa political appointees (wateule wa kisiasa) ambao hawajui chochote kuhusu sekta ya anga. Mtu akipewa nafasi hizo anatakiwa awe na ufahamu mkubwa kuhusu sekta ya anga.
Akijibu malalamiko ya marubani na wadau wa sekta ya anga jana, Mkurugenzi Mkuuu wa TCAA, Hamza Johari alisema kwa ufupi “kama Tapa wana changamoto, waje tujadiliane na kuzungumza, lengo letu ni kujenga ili sekta ya anga isonge mbele.”
Huduma mbovu za dharura
Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) limetoa mpango wa kushughulika na dharura katika viwanja vya ndege vilivyopo karibu na bahari, maziwa au maeneo oevu.
Mpango huo unalenga kupunguza madhara wakati wa dharura hasa kuokoa maisha ya watu. Mpango huo umeweka utaratibu wa kuratibu mwitiko wa vyombo vya viwanja vya ndege na vile vinavyozunguka jamii kusaidia wakati wa dharura.
Moja ya matakwa hayo ni kwa viwanja vya ndege vilivyo karibu na maeneo ya maji au oevu mpango wa wa kushughulikia dharura unatakiwa uhusishe uanzishwaji na ukaguzi wa mara kwa wa huduma za uokoaji.
Miundombinu muhimu katika kutekeleza hili ni uwepo wa kituo cha kushughulika na dharura, chumba cha mawasiliano ya simu na kitengo cha mawasiliano.
Viwanja vya ndege vya Mwanza, Bukoba, Mafia na Zanzibar viko karibu kabisa na bahari au Ziwa Victoria, hivyo kulazimika kukidhi vigezo vya ICAO.
“TCAA ilitakiwa kuwekeza kwenye safety (usalama) ili iwe na rescue coordination centre (kituo cha kuratibu uokoaji), vifaa vya uokoaji, mafunzo kwa wazamiaji waokoaji na vifaa vya uokoaji kwa ujumla lakini wenyewe wanaishia kwenye vikao Bagamoyo kula posho.
“Hakuna helikopta, hakuna wazamiaji waliofundishwa kuokoa watu waliozama majini. TCAA haijawahi kuweka mkakati wa ku-invest kwenye hili. Hapa huwezi kumlau Rais au waziri, wana watendaji wao. Tulitakiwa tuwe na boti za uokoaji zilizo tayari kwa kazi za dharura,” alisema Iqbal.
Kuhusu uwekezaji katika uokozi wa dharura, Johari alisema TCAA inatekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo udhibiti, lakini wamelipokea suala hilo na watashirikiana na mamlaka husika ili kuboresha eneo hilo, akisema ni somo kwao pia.
Kuanguka ndege
Iqbal haamini kuwa rubani wa ndege iliyopata ajali alifanya uamuzi wa kuishushwa Ziwa Victoria ikiwa ni harakati za kujiokoa. Anasema kuna uwezekano mkubwa ndege hiyo ilimshinda akijaribu kuinyanyua juu zaidi.
“Haja-land (hajatua) kwenye maji, ninavyo-assume (dhani) mimi. Sasa kwa nini ameanza kushukia pua, ni swali muhimu sana kujiuliza.
“Naona alifanya uamuzi ya kunyanyua ndege alipokuta dhoruba na pale ndipo performance (utendaji wa ndege) ikashindwa kufanya kazi, hiyo ni kawaida, ndege ina wind shiver na micro burst, ndio haikupita muda na kutoa tahadhari, alijua ataruka atapaa juu angani lakini nguvu ya thunderstorm (dhuruba) and upepo unaweza kuitupa chini ndege umbali wa futi 3,000 hadi 4,000 kwa dakika.
Kwa hiyo kilichotokea ni makosa juu ya makosa, kuanzia hapa Dar es Salaam kwa yule aliye-release hiyo nsege hali ya hewa ikiwa mbaya.
Rais Samia aingilie kati
Iqbar amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati kwa kukutanisha Tapa na TCAA kujadili maendeleo ya sekta ya anga.
Jana, Johari alifanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa tayari timu watalaamu ya uchunguzi kuhusu ajali hiyo inaendelea na kazi.
Alisema taarifa ya awali wa uchunguzi wa ajali hiyo itatolewa ndani ya siku 14, nyingine siku 30 na ikichelewa zaidi haitazidi miezi 12.
Alisema uchunguzi ajali hiyo ulianza tangu Novemba 6 mwaka huu.
“Timu hiyo (ya uchunguzi) ipo eneo la tukio imeshaanza kazi na baada ya kukamilisha uchunguzi wao watatoa maelezo ya awali yatatolewa ndani ya siku 14 kwa mujibu wa sheria, labda kuwepo kwa vitu vingine vitakavyowachelewesha.
“Baada ya hapo itafuata ripoti kamili ya uchanguzi itakayotolewa ndani ya siku 30, labda kuwepo na vitu vitakavyowachelewesha, lakini kwa mujibu wa kanuni ya 18 ya sheria ya uchunguzi za ajali za ndege za mwaka 2017 ripoti kamili inatakiwa itolewe ndani miezi 12,” alisema.
Mbali na hilo, Johari alisema licha ya kutokea ajali ya ndege ya Precision Air bado Uwanja wa Ndege wa Bukoba upo salama na amewatoa hofu Watanzania wanaotumia usafiri wanaolekea mkoani humo.
“Timu hiyo ipo eneo la tukio imeshaanza kazi na baada ya kukamilisha uchunguzi wao watatoa maelezo ya awali yatatolewa ndani ya siku 14 kwa mujibu wa sheria, labda kuwepo kwa vitu vingine vitakavyowachelewesha.
“Baada ya hapo itafuata ripoti kamili ya uchanguzi itakayotolewa ndani ya siku 30, labda kuwepo na vitu vitakavyowachelewesha, lakini kwa mujibu wa kanuni ya 18 ya sheria ya uchunguzi za ajali za ndege za mwaka 2017 ripoti kamili inatakiwa itolewe ndani miezi 12,” alisema.
Akizungumzia uzoefu wa kurusha ndege, mkuu wa kitengo cha udhibiti wa ubora wa ndege wa TCAA, Noel Komba alisema ndege inavyotoka Dar es Salaam, inaongozwa kama kawaida na mwongoza ndege hadi umbali fulani. Alisema ikifika eneo la Mwanza anakabidhiwa mtu wa mkoa huo mwenye jukumu la kuongoza ndege viwanja vya Mwanza, Geita, Buzwagi, Musoma, Shinyanga na Bukoba.
“Sasa utaratibu wa waongoza ndege kama unavyojua rubani anakuwa yupo juu, anavyoshuka kwenda Bukoba anapewa huduma na waongoza ndege ili kupishanisha na ndege zingine ikiwemo kumweleza hali ya hewa ya Bukoba.
“Huyu mwongoza ndege ana mitambo inayomwezesha pia kuwasiliana na rubani, pia kuna rada inayosaidia kuiona ndege, anamuongoza hadi rubani atakaposema ninauona uwanja wa Bukoba, akiripoti hivyo mwongozaji anamjibu sawa sasa tua, mengine yanabaki kwa rubani,” alisema Komba.
Mwananchi