MABOSI wa Simba wamekerwa na kitendo cha timu yao kudondosha pointi kwenye mechi za ugenini na wamekubaliana kwamba hakuna namna dirisha dogo la usajili lazima watumie pesa timu irudi kwenye ubora wake katika baadhi ya maeneo.
Kwenye mahojiano na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema jambo la kwanza uongozi umekubaliana kutenga pesa ya maana ili kuwasajili wachezaji watakaokuwa wanawahitaji hata kama wakiwa na mikataba na timu nyingine na watafanya pia uamuzi mgumu.
Barbara alisema dirisha dogo la usajili mara nyingi wachezaji wazuri wanakuwa kwenye mikataba kuwapata inahitaji pesa ndefu kuvunja mikataba yao kutokana na hali ilivyo wanakwenda kulifanya hilo.
Alisema wanahitaji wachezaji wapya wachache wenye ubora wa hali ya juu ili kuongeza makali ya timu haswa mzunguko wa pili pamoja na kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tunatenga bajeti ya kutosha ili kuwapata wachezaji wenye ubora kama kila eneo ambalo limekuwa na upungufu ndani ya kikosi chetu haswa kwenye huu mzunguko wa kwanza,” alisema Barbara ambaye ndiye kiongozi wa kike mwenye cheo kikubwa zaidi kwenye soka la Tanzania kwa sasa.
“Kutokana na maboresho hayo kuna maamuzi magumu yatafanyika ndani ya timu ikiwemo baadhi ya wachezaji huenda tukaachana nao kwenye dirisha hili dogo la usajili na tunafanya yote kwa malengo ya kufanya vizuri kwenye mashindano yote kama malengo yetu yalivyo,”alisema Barbara ambaye ana sapoti kubwa ya vigogo wazoefu ndani ya Simba na soka la Afrika.
“Baada ya maboresho ya kikosi tunakwenda kuweka nguvu nyingine kwenye benchi la ufundi siku si nyingi kuna mtaalamu mwingine tutamtangaza anakuja kwa ajili ya kuongeza nguvu hapo,” alisema bila kuingia kiundani ni nafasi zipi watasajili na idadi ya wachezaji.
“Tutakaa na wachezaji wetu chini kuongea nao kila mmoja kufahamu tathamni ya Simba kila mmoja anatakiwa kupambana kadri anavyoweza ili kuona timu inafanikiwa kwenye nyakati zote,” aliongeza kiongozi huyo ambaye awali aliweka wazi kwamba malengo ya kwanza ya Simba msimu huu ni kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Katika hatua nyingine Barbara alisema mashabiki wa Simba wanatakiwa kutulia kwani uongozi haupo tayari kuona timu hiyo inashindwa kufanya vizuri kwenye mashindano yote msimu huu na kwamba watafanya kila kinachowezekana.
“Uongozi hatupendezwi kuona timu yetu inashindwa kufanya vizuri kwani inakuwa ni nje ya malengo yetu tumekaa chini tumejipanga tunakuja na njia sahihi ya kubadilisha hili,” alisema Barbara ambaye masomo yake ya juu ya uchumi na maendeleo ameyasomea Marekani na Uingereza.
KANOUTE NDANI YA NYUMBA
Kiungo wa Simba, Sadio Kanoute aliyekosekana kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City ugenini kutokana na majeraha ya goti, amefanya mazoezi vizuri siku mbili tayari kuwakabili Polisi Tanzania Jumapili Uwanja wa Ushirika Moshi.
Kanoute miongoni mwa wachezaji waliopo na kikosi cha Simba Moshi kukosekana kwake kwenye mechi ya Mbeya City nafasi yake ya kiungo wa ukabaji alicheza, Jonas Mkude.
Kikosi cha Simba kumekuwa na muunganiko mzuri eneo la kiungo msimu huu akicheza mara kwa mara, Kanoute, Mzamiru Yassin na Clatous Chama ikitokeo mmoja wapo amekosekana kumekuwa na mapungufu si kama wakiwepo wote kwa pamoja uwanjani kwenye eneo hilo.
Alipoulizwa Kanoute alisema “Naendelea vizuri kiafya tofauti na ilivyokuwa hapo awali baada ya mchezo na Ruvu Shooting.”