KIUNGO wa Yanga, Gael Bigirimana hajawa na uhakika wa nafasi ya kucheza ndani ya kikosi hicho tangu amejiunga na Wanajangwani hao kwenye dirisha kubwa la usajili msimu huu lakini leo ameweka wazi sababu zinazomfanya asote benchi.
Kiungo huyo alitua Yanga na kutambulishwa na Rais wa klabu hiyo Hersi Said mbele ya wanachama waliohudhuria Mkutano mkuu wa klabu hiyo ulioambatana na uchaguzi wa viongozi, Julai 9,2022 na kupokelewa kwa shangwe kubwa.
Gael raia wa Burundi amesema mazingira na ubora wa kikosi cha Yanga kwa sasa hususani eneo la kiungo analocheza ndio sababu ya yeye mara nyingi kukaa benchi licha ya kuwa yupo fiti.
“Natamani kuitumikia Yanga kwa muda mrefu uwanjani na naamini nitafanya hivyo kila nikipata nafasi.
Mwanzo mazingira yalikuwa changamoto kidogo kuzoea lakini kwa sasa nimezoea na nipo tayari kwa mechi yoyote,” alisema Gael na kuongeza;
“Niko hapa ili kuifanya timu ifikie malengo, wanaopata nafasi mara kwa mara ni wachezaji wazuri hivyo si busara kuwazungumzia wao zaidi, kila jambo na wakati na mimi wakati wangu utafika nitacheza kwani naamini katika ubora wangu.”
Gael ambaye ni kiungo mkabaji aliyewahi kuicheza Newcastle United ya Ligi Kuu England na timu nyingine za Ulaya anakabiliwa na ushindani wa Namba kutoka kwa Yanick Bangala na Kharid Aucho ambao wamekuwa wakipangwa mara kwa mara kucheza eneo hilo.