Kijana mwenye umri wa miaka 20 mkazi wa Kijiji cha Kinazi Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, ametoa ombi kwa Watanzania, serikali na hata wataalam wa magonjwa ya upasuaji kumsaidia kutatua changamoto aliyonayo ya kutokuwa na jinsia ili awe kama wanadamu wengine.
EATV imefunga safari ya takribani saa moja kwa Pikipiki na kufika nyumbani kwao katika Kijiji cha Kinazi, lengo ni moja tu kuhakikishana anapata msaada wa changamoto yake kwanza yeye mwenyewe anasimulia.
Mzee Petro Bahona ni Baba mzazi wa binti huyo, amesema kwamba mara baada ya mtoto wake kuzaliwa iligundulika hana jinsia yoyote ile ya kike ama ya kiume.
Aidha binti huyu anaeleza magumu anayopitia na kukosa tabasamu kutokana na hali hiyo, na kusema kwamba afadhali hata angekuwa na elimu kwani ingemsaidia hata kuweza kuwasaidia wazazi wake.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Dkt. Lameck Mdengo anaeleza kuhusiana na mtu mwenye hali kama hiyo, amesema kwamba ni changamoto ya kiafya ambayo mtu huzaliwa nayo.