Bondia wa zamani wa uzito wa juu Goran Gogic (43) kutokea Montenegro amekamatwa juzi Jumanne (Novemba Mosi) jijini Miami-Marekani baada ya kushtakiwa kwa makosa ya kusafirisha tani 22 za Cocaine kwenda Ulaya.
Waendesha mashtaka wameeleza kuwa dawa hizo zilisafirishwa kutoka Colombia kupitia kwenye bandari nchini Marekani.
Ili kufanikisha usafirishaji, mashine za kunyanyulia mizigo mizito pamoja na nyavu zilitumika ili kupandisha dawa hizo kutoka kwenye boti za mwendo kasi kwenda kwenye meli za mizigo. Shughuli hizi zote zilifanyika usiku.
Kwa mujibu wa nyaraka za kortini Gogic alikuwa akisimamia usafirishaji wote huku akishirikiana na wasafirishaji wa Colombia , wafanyakazi wa melini na wabeba mizigo wa bandarini.
Kushtakiwa kwa bondia huyo, kumetokana na kukamatwa kwa mizigo mitatu ya dawa za kulevya mwaka 2019, mmojawapo ukiwa ni wa tani 19.8 ambao ni kati ya mizigo mikubwa katika historia ya Marekani.