Mandonga ambaye juzi aliwaacha vinywa wazi wadau wengi wa ndondi nchini kwa kumchapa kwa Knock Out (KO), Said Mbelwa bondia mwenye rekodi ya kucheza mapambano mengi anatajwa kuwa kwenye orodha ya mabondia namba moja nchini kwenye uzani wake.
Akimtolea mfano Mwakinyo, bondia nguli Emmanuel Mlundwa alisema, Mandonga anaelekea kwenye rekodi hizo.
“Renki zikitoka, anaweza kuwa namba moja, unapompiga bondia mwenye mapambano mengi inakupandisha kwa kasi sana,” alisema Mlundwa.
Kabla ya pambano hilo, Mbelwa alikuwa amepigana mara 86, ameshinda 47, amepigwa 34 na kutoka sare mara 5 akikamata namba mbili kwa ubora kwenye uzani wa light heavy nchini wakati Mandonga amepigana mapambano matano, ameshinda moja, amepigwa mara tatu na sare moja akiwa wa 19.
“Ni kama ilivyokuwa kwa Mwakinyo kabla ya kucheza na Eggington (Sam), hakuwa kwenye renki ya juu, lakini aliposhinda alipanda mara dufu, Mandonga ndiko anaelekea, matokeo haya yanaweza kumpandisha hadi nafasi ya kwanza,” alisema.
Katika pambano hilo, Mbelwa alipigwa KO raundi ya sita licha ya kumlalamikia refarii, Anthony Rutha alilimaliza yeye akiwa fiti kuendelea baada ya kuhesabiwa.
“Alilewa kwa ngumi, hakuwa na nguvu za miguu, japo ni kweli nilipomhesabia baada ya kuangushwa alisema anaendelea, ilikuwa lazima nimuokoe ili kuepusha madhara,” alisema Rutha.
Akilichambua pambano hilo, bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka alisema limechangizwa na Mbelwa kumdharau mpinzani wake.
“Inaonekana hakujiandaa vyema, Mandonga alijipanga, amebadilika sana na inaonyesha alifanya sana mazoezi.”
Mandonga alisema matokeo hayo ni matunda ya maandalizi bora huku akitamba; “Niliwahi kusema siku nitakapomvunja mtu taya ulingoni ndipo wataniheshimu, huu ni mwanzo tu,” alijinasibu Mandonga huku Mbelwa akiomba warudiane.