CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimefuta matokeo ya uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti Umoja wa Vijana Mkoa wa Simiyu na kusimamisha mchakato wa uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho katika mikoa ya Mbeya na Arusha.
Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amewaambia waandishi wa Habari mjini Dodoma leo Novemba 21 kuwa maamuzi hayo yametokana na dosari katika mchakato wa uchaguzi sambamba na tuhuma za rushwa.
Haikufahamika ni lini uchaguzi wa Mwenyekiti UVCCM Simiyu utarudiwa ama maamuzi ya mwisho kuhusu mchakato wa uchaguzi Mkoa wa Mbeya na Arusha yatafanyika.
Habarileo inafahamu kuwa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa umepangwa kufanyika Novemba 24 jijini Dodoma ambapo wajumbe 893 wamepangwa kuhudhuria.
Mkutano huo wa siku mbili unalenga pamoja na mambo mengine kufanya uchaguzi wa viongozi wa jumuiya ngazi ya taifa. Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Gilbert Kalima amesema nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, na wajumbe watano wa NEC ya CCM. Pia kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe sita wa Baraza Kuu la Wazazi taifa.
Wagombea waliopitishwa na vikao vya juu vya Chama cha Mapinduzi wanatarajiwa kuwasili jijini Dodoma leo Novemba 21 kujiandaa na uchaguzi huo.