KIUNGO fundi wa Simba, Clatous Chama amesema wapenzi na mashabiki wa timu hiyo wanatakiwa kutulia kwani ushindani wa Ligi Kuu Bara bado ni mkali licha ya kudondosha pointi tano hivi karibuni.
Kuhusu suala la kupewa adhabu ya kufungiwa mechi tatu, Chama alisema anayaheshimu maamuzi na anaamini kikosi cha Simba kina wachezaji wengi wanaoweza kuziba nafasi yake.
Alisema ataendelea kufanya mazoezi na timu ila ndani Simba kuna wachezaji wengi wenye uwezo wa kuziba tena bila shida yoyote.
“Benchi la ufundi litafanyia kazi hili na naimani kila kitu kitakwenda vizuri katika michezo ijayo ikiwemo kupata ushindi bila ya uwezo wangu, kwahiyo tunatakiwa kusahau ya nyuma na kungalia mbele,” alisema Chama na kuongeza;
“Kupoteza pointi tano kwenye kipindi cha hivi karibuni si jambo zuri kwetu lakini naamini ligi inaushindani hata aliyekuwa kileleni anaweza kupoteza zaidi ya hizo‚ kikubwa tunarudi kwenye mazoezi tunakwenda kukosoa zile changamoto zetu kulingana na maelekezo ya benchi la ufundi na tutarudi kwenye matokeo bora mfululizo.
“Simba ni timu kubwa inapokosa ushindi lazima mashabiki wake watakuwa hawapendezewi na jambo hilo kama wachezaji tunalitambua na kwenda kulifanyia kazi kwenye michezo ijayo.”
Chama amefungiwa michezo mitatu kwa kosa la kutosalimiana na wachezaji wa Yanga kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza kwenye ligi. Kukosekana kwa Chama kwenye mechi ya Singida Big Stars iliyochezwa Uwanja wa Liti na kuisha kwa sare ya bao 1-1, nafasi yake alitumika Kibu Denis kabla ya baadaye kuingia Peter Banda aliyekuja kufunga bao la kusawazisha.
Kuhusu kufungiwa kwa Chama, Kocha Mgunda alisema; “Wale waliocheza ni wachezaji wa Simba na mpira una matokeo bila kujali yupo nani, kukosekana mtu mmoja isiwe sababu.”