CEO wa SpaceX na Tesla, Elon Musk Mzaliwa wa Pretoria, Afrika Kusini ambaye ni Tajiri namba moja duniani na Boss mpya wa Twitter ametimiza ahadi yake ambapo leo rasmi ameirudisha hewani akaunti ya Twitter ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.
Kabla ya kumrudisha Trump Twitter, Musk aliwataka Watumiaji wa Twitter wapige kura ya kama wanahitaji Trump arudi Twitter au laah ambapo asilimia 52 ya waliopiga kura walisema NDIO arudi na asilimia 48 walisema HAPANA “Watu wameongea (kupitia kura) Trump anarudi Twitter”
Itakumbukwa muda mfupi tu baada ya kuinunua Twitter kwa USD Bilioni 44, Musk alimfukuza kazi Afisa Mkuu wa Sheria, Sera na
Uaminifu wa Twitter, Vijaya Gadde ambaye alifanya maamuzi ya kuifuta akaunti ya Twitter ya Trump, na uamuzi huo ukaashiria huenda akatimiza ahadi ya kumrudisha Trump Twitter.
Mwezi May mwaka huu Elon Musk alisema endapo ombi lake la kununua Twitter litafaulu na kupewa umiliki rasmi, atabatilisha marufuku ya Donald Trump kutoka Twitter na atamrudisha Trump Twitter akisema uamuzi wa Twitter kumfungia Trump ulikuwa upotovu wa kimaadili na wa kijinga mtupu.
Itakumbukwa mnamo Januari 2021, Twitter ilisema akaunti ya Trump ilisitishwa kabisa kutokana na hatari ya kuchochea ghasia zaidi kufuatia kuvamiwa kwa jengo la Capitol nchini Marekani.