Haina Mbambamba! Ndivyo utakavyoweza kusema baada ya Kamati ya Mashindano ya Yanga, kutoa ahadi ya nusu bilioni, yaani Sh 500Mil kwa mastaa wake kama watafanikiwa kuipeleka timu hiyo katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mastaa baadhi wa Yanga, Fiston Mayele, Khaliod Aucho, Yannick Bangala, Djigui Diarra, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Dickson Job, leo wanatakiwa kupambana watakapocheza mchezo wao wa kwanza wa Play-Off wa Shirikisho dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Yanga leo watajitupa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam katika mchezo huo wa Shirikisho watakaocheza dhidi ya Club Africain ya nchini Tunisia saa 10:00 Jioni.
Mmoja wa mabosi wa Yanga, ameliambia Championi Jumatano kuwa, viongozi hao wametoa ahadi ya Sh 250Mil kwa kila mchezo kati ya hiyo miwili wa nyumbani na ugenini, hivyo wakifanikiwa yote, basi watapatiwa fedha hizo.
Bosi huyo alisema kuwa lengo la kutoa ahadi hiyo ya bonasi, ni kuhakikisha wanaongeza hamasa ya wachezaji wao watakapokuwepo uwanjani wakiipambania timu.
Feisal Salum ‘Fei Toto’ akishangilia na Aziz Ki.
Aliongeza kuwa, kikubwa hawataki kuona kilichotokea katika Ligi ya Mabingwa Afrika cha kutolewa hatua ya kwanza, wakati wana kikosi bora na imara.
“Leo (jana) usiku viongozi hao walitarajiwa kukutana na wachezaji na benchi la ufundi mara baada ya mazoezi ya mwisho kufanyika.
“Kikao hicho kitahusisha chakula cha usiku cha pamoja, pia kufanya kikao kizito na wachezaji ambao wao ndio litakuwa jukumu lao la kupambana na kuamua matokeo.
“Katika kikao hicho kitaendana na ahadi ya bonasi ya wachezaji kwa kuanzia mchezo huu wa kwanza wa hapa nyumbani wameahidiwa Sh 250Mil na ule wa ugenini pia 250Mil ambao kama wakishinda utawapeleka makundi Shirikisho,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia hilo, Ofisa Habari wa timu hiyo, Ally Kamwe alisema kuwa: “Katika kila mchezo inakuwepo bonasi ambayo ni siri, hivyo kuelekea mchezo huo dhidi ya Club Africain ipo bonasi.”
MASTAA YANGA WAAPA
Uongozi wa Yanga umeweka wazi kuwa wachezaji wote wamekubaliana kufanya vizuri kwenye mechi za mtoano ili kufika mbali kimataifa.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliliambia Championi Jumatano, kuwa wachezaji wote wana morali kubwa kuelekea mechi zao za kimataifa na malengo ni kushinda.
“Wachezaji wamekubaliana kupata ushindi kwenye mechi zetu ambazo tutacheza kimataifa hivyo mashabiki wasiwe na presha wawe pamoja nasi kila hatua kwenye mechi zetu.
“Ushindani ni mkubwa na tunajua kwamba hakuna ambaye anapenda kuona tunakwama hivyo kila mmoja azidi kuwa pamoja nasi,” alisema Kamwe.