Hanje apasua 'jipu' Mahakamani, awataja Mnyika na Mbowe uteuzi wake




MBUNGE Viti Maalum, Nusrat Hanje, ameshauri suala lao la kupinga kuvuliwa uanachama wa Chadema, lirudishwe ndani ya chama hicho, kwani kuendelea kuwepo mahakamani ni kujidhalilisha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Nusrat ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, tarehe 4 Novemba 2022, mahakamani hapo mbele ya Jaji Cyprian Mkeha, wakati akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili Peter Kibatala, kuhusu malalamiko yake ya kufukuzwa Chadema.

Ni katika kesi Na. 36/2022, aliyoifungua yeye na wabunge wenzake 18, kupinga uamuzi wa Chadema kuwafukuza uanachama, wakidai haukuwa halali kwa kuwa hawakupewa nafasi ya kujitetea dhidi ya tuhuma zilizokuwa zinawakabili za usaliti.

Wakili Kibatala, ambaye ni kiongozi wa Jopo la Mawakili wa Chadema, alimuuliza Nusrat, kwa nini katika malalamiko yake hakuona ni suala la msingi mahakama hiyo kuamua madai ya chama hicho kwamba hakijawahi kumteua kwa sababu alikuwa gerezani.


Ambapo Nusrat alijibu akidai “ndiyo maana nimekuja kwenye mahakama hii sababu there is a lot (yapo mengi) ya kusema. Mimi sio mwendawazimu tunajidhalilisha ndiyo maana nimeomba turudi kwenye chama kuzungumza.”


Wakili wa Chadema, wakiongozwa na Peter Kibatala (katikati) wakiwa mahakamani
Pia, Wakili Kibatala alimhoji Nusrat kwamba, Chadema kupitia kiapo chake kinzani katika kesi hiyo, kinasema hakijamdhamini kuwa mbunge viti maalum.

Swali hilo lilimfanya Nusrat kuanza kutema nyongo, na kudai vyama vya siasa vinauwa ndoto za vijana huku akishangaa kwa nini chama chake kinakana hakijamdhamini ili Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC), kumteua kuwa mbunge viti maalum.


Nusrat amedai kuwa, ameshangaa kwa nini chama hicho kinamkataa wakati aliahidiwa kuwa atakuwa Mbunge Viti Maalum.

Alidai kuwa, hata alipokuwa gerezani akikabiliwa na shauri la jinai, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa chama hicho, walishiriki mchakato wa kumtoa.

“Kwanza nimeshangaa, katika chama nimekuwa- Promissed kuwa mbunge na nilikuwa kiongozi mwandamizi. Mwenyekiti na Katibu Mkuu wamekuja gerezani nimesaini wakasema you don’t have to worry (hupaswi kuogopa). Kuna vitu vingine tunashangaa vinakuja, nimekuwa- sponsored kwa mujibu wa mchakato na wanaofanya uteuzi ni tume,” amedai Nusrat.

Baada ya Wakili Kibatala kumaliza kumhoji maswali hayo, Wakili mwingine wa Chadema, Hekima Mwasipu alimhoji kuhusu fomu Na. 8 inayotolewa na NEC kwa ajili ya uteuzi wa wabunge viti maalum, ambapo alimuuliza kama anaifahamu.


Nusrat alijibu kuwa anaifahamu.

Wakili Mwasipu alimuuliza kama anafahamu chama kikishamteua mtu kuwa mbunge au jina lake likishaenda NEC, lazima ajaze fomu hiyo.

Wakili huyo alimuuliza kama aliijaza fomu hiyo, ambapo alijibu aliijaza. Kisha akamuuliza aliijazia wapi na nani alimpa fomu aijaze wakati alikuwa gerezani hadi usiku wa tarehe 23 Novemba 2020, alipoachiwa huru na kesho yake, Novemba 24, 2020 kwenda kuapishwa bungeni jijini Dodoma.

Nusrat alijibu akidai aliletewa gerezani na Mnyika kati ya mwezi Julai na Novemba 2020.

“Kwanza itambulike kwamba fomu zinazohusiana na masuala ya uchaguzi nililetewa gerezani na katibu mkuu wa chama John Mnyika. Na haikuwa kitu cha kushangaza sababu nilikiwa katibu mkuu wa vijana hivyo nimekuwa nikisaini nyaraka….,” amedai Nusrat.


Pia, Wakili Mwasipu alimhoji Hanje nani aliyempa taarifa ya yeye kwenda bungeni kuapishwa, ambapo alijibu akimtaja Mnyika na Mbowe.

“Ieleweke nilikuwa natembelewa na viongozi, mwenyekiti na katibu nikiwa gerezani na nimetoka gerezani nikawapigia simu wakaniuliza kama niko fit, nikawaambia niko fit. Nimepigiwa na viongozi wa chama akiwepo Mwenyekiti na katibu mkuu aliniambia tarehe 24 Novemba 2020 nikaapishwe na waliniambia watanitetea katika nafasi niliyogombea,” amedai Nusrat.

Katika hatua nyingine, Nusrat alihoji kwa nini viongozi hao walimuacha kwenye mataa.

“Nategemea katika hati yake ya kiapo waje kuthibitisha, mbona wameniacha kwenye mataa? Au pengine kuna wengine walitaka niwe mbunge wengine hawakutaka. Katibu Mkuu ndiyo aliniambia ngoma inaenda, nilitegemea aje aseme ilikuwaje,” amedai Nusrat.

Madai ya kwamba Mnyika alishiriki mchakato wa uteuzi wa wabunge viti maalum, yalianza kutolewa na Mbunge Viti Maalum, Grace Tendega, wakati anahojiwa mahakamani hapo, ambapo alidai kiongozi huyo wa Chadema, alitoa majina yake 10 likiwepo la Nusrat, akitaka asiachwe.
Jaji Mkeha ameahirisha kesi hiyo kwa muda ambapo Nusrat ataanza kuhojiwa maswali ya ufafanuzi kuhusu maswali ya dodoso aliyoulizwa na mawakii wa wajibu maombi.


Mbunge huyo viti maalum, aliapishwa na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, tarehe 24 Novemba 2020, ikiwa ni muda mfupi tangu aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, kumfutia mashtaka yaliyokuwa yanamkabili.



Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad