India yanasa kilo 61 za dhahabu ikiwamo ya Tanzania




Dar es Salaam. Maofisa wa forodha nchini India wamekamata kilo 61 za dhahabu zenye thamani ya randi 320 milioni (Sh9.18 bilioni) ikiwamo kwa wasafiri waliotoka Tanzania.

Watuhumiwa saba wamekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Mumbai wakiwamo wanawake wawili kutokana na sakata hilo lililohusisha matukio mawili.

Kwa mujibu wa gazeti la India Times la nchini humo, katika tukio la kwanza, maofisa hao waliwakamata wasafiri wanne waliokuwa wanatoka Tanzania wakiwa na kilo 53 za dhahabu na wengine watatu akiwamo bibi wa miaka 61 waliokuwa wanatoka Dubai wakiwa na kilo nane za madini hayo ya vito.

“Hiki ni kiasi kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa mara moja katika historia ya Idara ya Forodha ya Uwanja wa Ndege wa Mumbai,” limeandika gazeti hilo.


Katika ukamataji huo, wasafiri wanne waliobeba kilo 53 za dhahabu waliyoificha kwenye mikanda yao walikamatwa. Ingawa wasafiri wote ni Wahindi, wametokea Tanzania wakiwa wameifunga dhahabu hiyo kwenye miche ya kilo mojamoja.

Kwa ujumla, wasafiri hao wlaikamatwa wakiwa na madini yenye thamani ya randi 281.7 milioni (Sh8.08 bilioni).

Taarifa zinasema dhahabu hiyo ilifichwa kwenye mikanda iliyotengenezwa Falme za Kiarabu na walikabidhiwa na raia wa Sudan waliyekutana naye Uwanja wa Ndege wa Doha walikokuwa wanabadilisha ndege.


Maofisa wa forodha wamefanikiwa kuwakamata watu hao baada ya kuweka mtego kwa abiria wanaotoka mataifa fulani ya Afrika na Mashariki ya Mbali.

Kwenye mahojiano waliyofanyiwa, walisema walipewa mikanda hiyo na mtu waliyekutana naye Doha waliposhuka kwenye ndege ya Shirika la Ndege la Qatar wakitokea Tanzania. Hawakuwa wamesafirina mtu huyo kutokea Tanzania.

Watuhumiwa wote wanne wanashikiliwa wakisubiri kupandishwa kizimbani ndani ya siku 14 utaratibu utakapokamilika.

Kabla haujavunjwa Mei 2017, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) uliwahi kutangaza kubaini zaidi ya njia za panya 400 zinazotumika kutoroshea madini nchini hivyo hatua za makusudi zikachukuliwa kudhibiti mianya hiyo.


Kutokana na kuimarika kwa udhibiti ikiwamo kujengwa kwa ukuta kuzunguka midogo ya Tanzanite huko Mirerani mkoani Manyara, mwezi uliopita Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko alisema kuna mbinu mpya inatumika kutorosha madini nchini.

Dhahau hii imekamatwa ikiwa imepita miezi saba tangu Kampuni ya SJ Gold and Diamond ilipopanga kufanya maonyesho ya vitu kulitambulisha jiwe la rubi nyekundu la kilo 2.8 ililosema imelipata Tanzania kabla Serikali haijakanusha taarifa hizo.

Rubi hiyo yenye thamani ya Sh276 bilioni (dola 120 milioni za Marekani) ilidaiwa kuchimbwa katika Kijiji cha Winza wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.

Tanzania licha ya kutajwa kuwa na hazina kubwa ya madini, hainufaiki sana na rasilimali hizo kiasi cha wananchi wake kuendelea kuishi katika lindi la ufukara wakiwa hawana uhakika wa maji safi na salama wala umeme wa kutosha hata huduma za afya.


Akiwasilisha bajeti ya mwaka huu, Dk Biteko alisema hatua kadhaa zimechukuliwa ili kuimarisha ukusanyaji maduhuli na kudhibiti utoroshaji wa madini, kazi inayofanywa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Ofisi ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa na wilaya pamoja na raia wema.

“Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, madini ya Sh501.2 milioni yakiwamo dhahabu, vito, mchanga na madini ya viwandani yalikamatwa yakitoroshwa katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Manyara, Dodoma, Lindi, Geita, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza,” alisema Waziri Biteko.

Kilo nane, abiria watatu
Katika tukio la pili, maofisa hao wa forodha wamekamata kilonane za dhahabu zenye thamani ya randi 38.8 milioni (Sh1.11 bilioni) kutoka kwa abiria watatu wakiwamo wanawake wawili waliokuwa wanatokea Dubai.

Hawa walikuwa wanasafirisha dhahabu hiyo ikiwa imesagwa na kuwa unga uliofichwa kwa kushonewa kwenye jeans eneo la kiunoni mwa kila mmoja akiwamo mwanamke wa miaka 61 anayetembea kwa kiti cha wagonjwa (wheelchair).

Wote watatu nao, wanashikiliwa na polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad