Ishu ya Saido, Geita Gold iko Hivi, George Mpole Aendelea Kukaza



VIONGOZI wa Geita Gold wamemalizana na kiungo wake mshambuliaji, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ baada ya kutoweka kambini na hata mastaa wengine waliokuwa hawapo wamerejea.

Mbali na Saido mastaa wengine waliotimka kambini kutokana na madai mbalimbali ni Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Hussein Bakari, Samson Sebusebu na Oscar Masai. Lakini wameshayajenga na viongozi kimyakimya na wamerejea isipokuwa George Mpole.

Saido, nyota wa zamani wa Yanga aliondoka kwenye kambi ya timu hiyo kwa kile kilichodaiwa kuidai klabu hiyo fedha zake, lakini wamekaa chini na mchezaji huyo juzi usiku na kukubaliana kumlipa stahiki zake zote.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Katibu Mkuu wa timu hiyo,Liberatus Pastory alisema hakuna changamoto iliyopo baina yao na nyota huyo huku akiweka wazi yoyote anayekiuka taratibu zao atachukuliwa hatua za kinidhamu.


“Hakuna mchezaji mkubwa zaidi ya klabu hivyo niwatoe hofu tu mashabiki zetu kwamba tuko kwenye mstari mzuri na tusikubali kurudishwa nyuma na watu ambao wasiotutakia mema,” alisema Liberatus na kuongeza;

“Kuhusu Mpole ni kweli hayupo na timu kwa sababu ana matatizo yake ya kifamilia ingawa waliobaki wote wamerejea.”

Kwa upande wa Saido alisema hana tatizo na uongozi wake na kilichotokea kwake hawezi kukizungumzia sana isipokuwa kazi yake ni kuhakikisha anafanya vizuri kwenye kila mchezo na kuisaidia timu yake.


Awali Mpole alisema anashangazwa na kauli za viongozi zinazoendelea juu yake kwani anaumwa ila wao kwa upande wao hawamjali kwenye matibabu jambo ambalo Pastory alilikanusha vikali na kudai sio la kweli.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad