Songwe. Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za kulevya (DCEA) Gerald Kusaya amesema ndani ya mwaka mmoja wamekamata kilo 9,680 za dawa za kulevya aina ya bangi.
Amesema hayo leo Alhamisi, Novemba 17 katika Mkutano wa wadau kuhusu elimu ya kupambana na matumizi ya dawa za kulevya uliofanyika Songwe huku akiongeza hekali 21 za bangi zikiteketezwa ndani ya mwaka mmoja.
"Katika kipindi cha mwaka mmoja tumeweza kukamata watuhumiwa 2,408 nchi nzima wanaotokana na hii biashara au matumizi ya dawa za kulevya, huku kilo 11,974.4 za dawa za kulevya zikishikwa na hiki ni kiwango kikubwa sana.
Ameongeza dawa aina ya heroine ikishikwa kilo 230.66, Cocaine gramu 366 lakini eneo la bangi ndio linaongoza na mirungi imeshikwa kilo 4,397.7.
Hata hivyo amesema Mkoa wa Dar es Salaam, Tanga na Pwani ndio vinara wa kuingiza na kutumia dawa za kulevya.
"Mikoa hiyo inaongoza kutokana na jiografia ya nchi ilivyo sababu dawa nyingi tunazokamata zinakuwa zimeingizwa kwa njia ya maji (bahari) ambapo udhibiti wake unakuwa na changamoto kutokana na uwepo wa ukubwa wa bahari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika linalojihusisha na Kupambana na Ukimwi, HJF Medical Research International (HJFMRI), Sally Chalamila amesema mkutano huo unasaidia wengi kupata elimu katika kupambana na matumizi ya madawa ya kulevya ili kuzuia maambukizi ya Ukimwi kwa waraibu wa dawa hizo na jamii.
"Unapopambana na mambo ya madawa inapasa tusioneane haya sababu mwisho wake unakwenda kuongeza idadi ya waathirika wa Ukimwi.
"Tusipodhibiti dawa za kulevya hata HIV itaendelea kuwepo sababu Tunduma ambapo ndio mpakani kuna makisio ya watumiaji 250 hadi 300," anasema Sally.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba amesema, "Lazima tuchukue hatua ngumu katika hili maana mtu anapokuwa mwathirika anakuwa hana maana yoyote kwa jamii wala serikali sababu hazalishi chochote na hawezi kulima wala kufuga."