Wakili wa Chadema, wakiongozwa na Peter Kibatala (katikati) wakiwa mahakamani
BAADHI ya wabunge viti maalum wameendelea kudai katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu jijini Dar es Salaam, kwamba Chama cha Chadema kiliwateua kushika wadhifa huo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Madai hayo yameibuliwa tena Kwa mara ya tatu leo Jumanne, tarehe 8 Novemba 2022 na Mbunge Viti Maalum Cecilia Pareso, akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa Chadema, Peter Kibatala, kuhusu malalamiko yake ya kufukuzwa Chadema kinyume Cha Sheria.
Ni katika kesi Na. 36/2022, iliyofunguliwa na Pareso akishirikiana na wabunge wengine 18 viti maalum wakiongozwa na Halima Mdee, dhidi ya Chadema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kupinga mchakato uliotumiwa na chama hicho kuwafukuza wakidai haukuwa halali kwa kuwa hawakupewa nafasi ya kusikilizwa.
Mbele ya Jaji Cyprian Mheka, Kibatala alimhoji Cecilia ni kweli ama sio kweli kwamba Chadema kupitia hati yao ya kiapo kinzani waliyowasilisha mahakamani hapo wanadai hawajamteua kuwa mbunge viti maalum.
Ambapo Cecilia alijibu akidai ni kweli Chadema kupitia hati yake ya kiapo kinzani, wanasema hivyo lakini ukweli ni kwamba kwa mujibu wa utaratibu hakuna mtu anayeweza kujiteua kuwa Mbunge.
Cecilia anaungana na wabunge wenzake viti maalum, Nusrat Hanje na Grace Tendega, kudai Chadema kilihusika katika mchakato wa kuwateua kushika wadhifa huo.
Wabunge hao wametoa madai hayo katika nyakati tofauti, wakati wanaulizwa maswali ya dodoso kuhusu malalamiko waliyowasilisha kwenye hati zao za viapo, kwamba Chadema haikuwapa nafasi ya kuwasikiliza dhidi ya tuhuma za kujiteua na kujipeleka bungeni, ambazo zinawakabili.
Awali, akiulizwa maswali hayo na Wakili Kibatala, Ceilia alidai hakupata nafasi ya kusikilizwa mbele ya kikao Cha Kamati Kuu ya Chadema Cha tarehe 27 Novemba 2020 kilichofanyika jijini Dar es Salaam, kwa kuwa alikuwa jijini Dodoma na kwamba aliomba aongezewe muda wa wiki Moja ambapo ombi lake lilikataliwa.
Hata hivyo, Wakili Kibatala alimhoji Kamati Kuu ya Chadema ingejuaje kwamba yeye alishindwa kufika mbele ya kikao hicho Kwa kuwa alikuwa Dodoma bila ya kuieleza.
Cecilia alijibu akidai hawakutaka kujua wapi alipo.
Cecilia alidai, alipokea wito wa kufika mbele ya kamati hiyo tarehe 25 Novemba 2020 kupitia mtandao wa WhatsApp, akiwa Dodoma.
Ambapo Wakili Kibatala alimhoji wapi mahakama hiyo ikiangalia itapata uthibitisho kwamba kipindi hicho alikuwa Dodoma.
Alijibu akidai kupitia ushahidi wa barua yake kwenda Kwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akimuomba amuongezee muda. Barua hiyo ameiwasikisha mahakamani kama sehemu ya ushahidi wake.
Cecilia anaendelea kuhojiwa maswali na Wakili Kibatala, mbele ya Jaji Mkeha.
Katika kesi hiyo iliyofunguliwa na Mdee na wenzake 18, baada ya tarehe 11 Mei 2022, Baraza Kuu la Chadema kutupilia mbali rufaa zao za kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kuwafukuza, wanaomba mahakama ifanye mapitio dhidi ya mchakato uliotumika kuwafukuza kama ulikuwa halali au lah