Kocha Matola "Naondoka Simba Sasa"




KOCHA Msaidizi wa Simba, Seleman Matola amelithibitishia Mwanaspoti kwamba anaondoka kwenye benchi la ufundi la timu hiyo kwa muda akapige shule kidogo.

Matola ambaye ni nahodha wa zamani wa Simba na Taifa Stars, amepata fursa ya kwenda kusoma kozi ya leseni A ya CAF, ataanza Novemba 21 ambapo atasoma kwa wiki mbili, kisha atarejea kikosini hapo kwa kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo aliyoyapata. Hiyo inamaanisha kwamba Matola hatokuwepo mpaka mwanzoni mwa mwezi Desemba.

Matola ambaye aliwahi kucheza Supersport ya Afrika Kusini amesema; “Nisingeweza kukataa fursa hiyo, lakini sitaacha kuitakia mema timu yangu, nitakuwa nawasiliana na kocha, kuhakikisha tunashauriana ili Simba ibaki kuwa imara kwa muda wote inapocheza ligi ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Nilishaongea na viongozi kila kitu kuhusu kozi hii, naamini watakuwa wanalifanyia kazi suala hilo, Simba ni klabu kubwa itaweka sawa kila kitu, zaidi ya hayo yote namshukuru Mungu kupata fursa hiyo na uzuri nitakuwa narejea kwenye klabu yangu kufanya mafunzo ya vitendo.”


Simba kwa kipindi hiki haina kocha wa makipa, baada ya Mwarami Mohamed kutokuwepo kikosini kuanzia mechi yao iliyopita dhidi ya Singida Big Stars ikitoka kwa sare ya bao 1-1, ikielezwa ana ‘matatizo ya kifamilia’.

Matola ambaye ana leseni B ya ukocha anakwenda kusoma kozi nyingine ya leseni A ya CAF nje ya Jiji Dar es Salaam ambapo atashindwa kufanya majukumu mawili kwa wakati mmoja.

Mabosi wa Simba watalazimika sasa kuboresha benchi la ufundi kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma kocha huyo alipokwenda kusoma timu ikiwa chini ya Didier Gomes ambapo alitafutiwa msaidizi wake Thierry Hitimana na baadaye Matola aliungana nao alipomaliza masomo yake.


Habari za ndani kutoka Simba pia zinaeleza kwamba kipa wao wa zamani Juma Kaseja huenda akala shavu kwa kipindi hiki ingawa bado linaendelea kujadiliwa suala lake. Kaseja kwasasa ni kocha wa makipa wa Taifa Stars na timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 23 ‘Ngorongoro Heroes’.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa upande wa kocha wa viungo ambaye nafasi yake ilikuwa wazi kwa muda mrefu tayari amepatikana ingawa hajatangazwa ingawa Mwanaspoti linafahamu kwamba anaweza akatangazwa muda wowote kuanzia sasa.

Kwa mara ya mwisho Simba ilikuwa na mtaalamu wa viungo Sbai Karim kutoka Tunisia aliondolewa pamoja na kocha Maki Zoran na kocha wa makipa alikuwa Mohamed Rachid raia wa Morocco.

Endapo uongozi wa klabu hiyo hautachukua hatua za haraka, watampa kazi ngumu Juma Mgunda kusimamia benchi hilo katika mechi dhidi ya Mbeya City (Novemba 23), Polisi Tanzania (Novemba 27), Coastal Union (Desemba 3), wakati mechi inayofuata dhidi ya Geita Gold itakuwa ni Desemba 18.


Hata hivyo, mabosi wa Simba walipotafutwa ili kuelezea hali hiyo ya benchi la ufundi simu zao za mkononi hazikupokelewa huku ikielezwa kuwa walikuwa kwenye kikao kizito cha ndani.

Simba imepania kufanya vizuri msimu huu hususani kimataifa ambako lengo ni kwenda nusufainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad