Mbinu hiyo ni ya kupata ushindi wa mabao mengi nyumbani, ambayo inatumiwa na Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda hadi akafanikisha timu yake kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Kesho Jumatano saa 10:00 jioni, Yanga inatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam kuvaana na Club Africain kabla ya wiki moja kurudiana.
Yanga wanapambana na Waarabu hao kusaka nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuondoshwa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na Spoti Xtra, Nabi alisema mashindano hayo ya kimataifa ili ufuzu hatua inayofuatia ni lazima uutumie vema uwanja wa nyumbani kwa kupata matokeo mazuri ya ushindi.
Nabi alisema katika kuelekea mchezo kesho, amewaambia wachezaji wake anahitaji ushindi wa mabao zaidi ya mawili kama kweli wanatakiwa kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.
Aliongeza kuwa, anaamini kama wakipata ushindi mkubwa nyumbani, basi utawafanya wapinzani wao kucheza kwa presha kubwa watakapokuwa kwao.
“Kutolewa katika hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kumenipa funzo mimi pamoja na wachezaji wangu, bila ya kusahau viongozi wetu.
“Kiukweli katika Ligi ya Mabingwa Afrika tulishindwa kufanya vizuri kwa kukosa matokeo mazuri nyumbani. Ninaamini tungepata ushindi wa mabao zaidi ya mawili, basi tungevuka hatua inayofuatia.
“Hivyo basi safari hii tumejipanga kupata matokeo bora mchezo huu wa kwanza ili kujihakikishia nafasi ya kumaliza kazi tutakapokuwepo ugenini,” alisema Nabi.
Yanga wakati inakwama hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Al Hilal ya Sudan, nyumbani ilitoka sare ya 1-1, ugenini ikafungwa 1-0.
Kabla ya mchezo huo, hatua ya awali, ilicheza dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini, mechi zote zilichezwa Uwanja wa Mkapa, Yanga ikashinda kwa jumla ya mabao 9-0.