Dar es Salaam. Wakati mkandarasi mradi awamu ya tatu ya mabasi yaendayo haraka ’mwendokasi’ barabara ya Gongo la Mboto akiwa tayari ameanza kazi, miundombinu ya mradi huo inatarajiwa kufika hadi Chamazi.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Novemba 15,2022 jijini humo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Edwin Mhede, alipokuwa akiwasilisha taarifa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angellah Kairuki katika hafla ya uzinduzi wa bodi ya Ushauri ya Dart.
Mhede amesema hatua hiyo inakuja baada ya kufanya utafiti na kugundua kuna uhitaji wa usafiri huo katika maeneo hayo hivyo badala ya mradi wa awamu hiyo ya tatu kuishia Gongolamboto, sasa utafika hadi Chamazi na utaungana na ule wa barabara ya Mbagala.
“Matamanio yetu ni mradi ukitoka Gongo la Mboto uende Chanika, ukaunganishwe na ile njia ya kutokea Chamazi ili ifungamishwe na BRT awamu ya pili ambayo ni barabara ya Mbagala.
"Kwa kuunganisha barabara hizo, tutafikia yale malengo ya kuwaondolea adha ya usafiri wakazi wa jiji la Dar es Salaam ambayo ni kiu ya Dart siku zote katika utekelezaji wa majukumu yake," amesema Mhede.
Kwa upande wa ruti ya Kigogo-Matumbi- Tabata Segerea, amesema tayari mfadhili wa kutekeleza mradi huo ameshapatikana na timu ipo kazini ikifanya tathimini kwa watu watakaopisha mradi huo.
Akieleza mafanikio ya mradi wa Dart amesema umesaidia kupunguza muda wa watu kusafiri kutoka saa tatu hadi dakika 45 na pia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kutokana na kupunguza msongamano wa magari maeneo ambapo mabasi hayo yanapita.
Kwa upande wake, Waziri Kairuki aliwapongeza Dart kwa kazi ambayo wamekuwa wakiifanya ya kupunguza tatizo la usafiri katika jiji hilo licha yakukabiliwa na changamoto mbalimbali.
Kuhusu bodi hiyo ya ushauri, Waziri Kairuki aliitaka ikahakikishe inasimamia fedha za miradi iendane na thamani ya fedha inayotolewa na serikali na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Aidha kwa upande wa Dart aliwataka kupitia mara kwa mara sheria na kanuni zilizounda wakala huo ili kuendana na wakati wa sasa.
"Miaka 15 tangu kuanzishwa kwa wakala huu sio haba,yapo mengi yamepita hapo katikati hivyo mambo hayawezi kuwa yaleyale ,jitahidini mara kwa mara kupitia sheria zenu ili kuendana na wakati,” amesema Kairuki.