Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima amekamatwa kwa tuhuma za rushwa.
Ofisi ya kupambana na rushwa nchini humo inasema kuwa kati ya Machi na Oktoba mwaka jana, alipokea zaidi ya dola 280,000 na vitu vingine kama malipo baada ya kusaidia kampuni mbili kupewa kandarasi za serikali.
Taarifa kutoka kwa ofisi hiyo inasema Bw Chilima atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka kadhaa yakiwemo makosa matatu ya ufisadi.
Hapo awali alihojiwa na wachunguzi kutoka ofisi hiyo lakini hajazungumzia madai hayo.
Chilima aligombea kiti cha urais mwaka 2019 lakini akashika nafasi ya tatu katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.
Baadaye aliungana na Rais wa sasa Lazarus Chakwera katika kama mgombea mwenza. Lakini uhusiano wa hivi karibunu kati ya Makamu wa Rais na Bw Chakwera umezorota kutokana na shutuma za ufisadi na upendeleo serikalini.
Bw.Chilima amewahi kufanya kampeni katika jukwaa la kupinga ufisadi akiahidi kumaliza miongo kadhaa ya ulafi serikalini na kumaliza umaskini katika mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani.