Marudiano, Yanga yawekewa Sh600 milioni mezani




YANGA juzi ilibanwa na Club Africain na kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza wa play-off ya Kombe la Shirikisho Afrika, uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini mastaa wa timu hiyo wamebakiwa na dakika 90 za ugenini ili kujihakikisha zaidi ya Sh 600 milioni.

Fedha hizo ni kwa timu itakayoingia makundi ya michuano hiyo, ingawa Yanga italazimika kupambana kiume na kupata angalau sare yoyote ya mabao katika mchezo huo utakaopigwa Jumatano ijayo kuanza saa 1:00 usiku.

Katika mchezo huo, Watunisia walikuwa wakijiangusha ovyo na kuwavaa wachezaji wa Yanga kila mara kutafuta faulo sambamba na kupaki basi, jambo lililowapa ugumu nyota wa Yanga kupenya kusaka mabao, licha ya kutengeneza nafasi kadhaa ambazo hazikuwa na madhara makubwa.

Ni mchezo ambao wageni walionekana kucheza kwa hesabu zaidi huku muda mwingi wakijaribu kupoteza muda wakilinda matokeo hayo ambayo yanawaweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.


Yanga ambayo ilionekana kutawala mchezo kwa muda mrefu, ilitengeneza nafasi chache ambazo ilishindwa kuzitumia mfano ile ya dakika ya 70 ambayo Fiston Mayele aliachia shuti kali la mguu wa kulia lililookolewa na kipa wa Club Africain.

Kipindi cha kwanza hakikuonekana kuwa na hatari nyingi kwa kila upande hasa kwa wageni ambao walionekana kuwaachia Yanga umiliki wa mpira kwa muda mrefu huku wao wakijaza idadi kubwa ya wachezaji katika eneo la ulinzi.

Tofauti na matarajio ya wengi, Yanga haikuonekana kutumia faida hiyo ya wapinzani kucheza kwa kujilinda ambapo ilitumia muda mwingi kupiga pasi za pembeni na za nyuma huku mara kadhaa ikijaribu kupiga mipira ya juu ambayo iliokolewa vyema na Club Africain.


Hali hiyo iliendelea hadi mwamuzi Alvacao Celso kutoka Msumbiji alipopuliza filimbi ya mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kumfanyia mabadiliko Tuisila Kisinda na kumuingiza Ducapel Moloko ambayo angalau yaliongeza uhai mbele ingawa bado ilionekana kukosa ubunifu katika eneo la mwisho pindi walipokuwa wanashambulia.

Mabadiliko mengine kwa Yanga katika mchezo huo yalikuwa ni kuwatoa Djuma Shaban na Bernard Morrison na kuwaingiza Farid Musa na Heritier Makambo lakini mabadiliko hayo hayakuzaa matunda.

Katika mchezo huo, refa Alvacao aliwaonyesha kadi za njano wachezaji Noureddine Farhat, Ahmed Khalil na Nadem Ghandri kwa rafu walizocheza kwa wachezaji wa Yanga pamoja na maofisa wawili wa Club Africain kwa utovu wa nidhamu walioonyesha wakiwa kwenye benchi.


Yanga itaifuata Africain ikiwa na kumbukumbu isiyovutia ya mechi za mwisho za raundi za awali za michuano ya Kombe la Shirikisho 2008 na 2015 na ule wa play-off katika ardhi ya nchi za Afrika Kaskazini, licha ya kocha msaidizi, Cedric Kaze kusema mechi haijaisha watazitumia dakika 90 zilizobaki kuhakikisha wanatinga makundi ya michuano hiyio kwa mara ya tatu baada ya 2016 na 2018.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad