KINARA wa mabao Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto' ametazamwa kwa jicho la tatu kwamba akiendelea kudumu na kiwango atazidi kujiandikia heshima ya kukumbukwa miaka ijayo kama ilivyo kwa baadhi ya wakongwe, ambao walifanya makubwa enzi zao.
Mastaa wa zamani wa Simba na Yanga, walisema mchezaji anayepitia klabu hizo kongwe akifanya makubwa anabakia kwenye vitabu vya historia ya kusimuliwa vizazi na vizazi.
Straika wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein 'Mmachinga' alisema kiwango cha Fei Toto kimekuwa na muendelezo, huku akimtaka kutojisahau na badala yake kuongeza bidii ili kujiandikia historia yake.
"Na sisi nyakati zetu, tulikuwa mastaa kweli kweli, tukafanya bidii tunakumbukwa hadi sasa, hilo ndilo anapaswa kulifanya Fei Toto na wengine ambao wanajitambua wamefuata nini kwenye soka," alisema.
Mtazamo wake ulikwenda sambamba na beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa aliyesema Fei Toto ni kati ya vijana wa Kitanzania wanaojituma na kutambua soka linahitaji nini kwenye miguu yao.
"Mfano mzuri waige kwa wachezaji wa zamani ambao majina yao yana nguvu hadi sasa kwenye jamii, siyo kwamba yamejengwa hivi hivi bali walifanya kazi kwa bidii inayoishi licha ya wao kustafu, siyo Fei Toto pekee bali nawashauri na wengine kuthamini nafasi wanayopata ndani ya klabu hizo," alisema.
Wakati aliyekuwa straika wa Yanga, Said Bahanuzi yeye alimshauri Fei Toto kutolewa sifa, bali aendelee kuwa mtu wa kazi "Ukiwa ndani ya klabu hizo unaweza usione faida ya kuzitumia fursa, pindi unapoondoka ndipo unajifunza mengi, hivyo wakati mwingine wajifunze kwetu ambao tupo nje ya kazi."
Msimu uliyopita Fei Toto alimaliza na mabao sita na asisti nne, ambapo kwa sasa anamiliki mabao manne.