KWA mujibu wa Idara ya Tafiti za kidunia, madaktari ndio watu wanaoaminika zaidi duniani. Wanabeba 54% kwa kuaminika. Wakifuatiwa na wanasayansi wanaoaminika kwa 51%, huku waalimu wakishika nafasi ya tatu kwa kuwa na 43%.
Kiungo wa kimataifa wa Uganda na Yanga, Khalid Aucho amepewa jina la Daktari kuashiria imani waliyonayo wapenzi na mashabiki kutokana na uwezo wake. Mashabiki wake wanamwita Daktari Aucho. Ni heshima kubwa sana kwake.
Ni imani kubwa sana kwake kutoka kwa mashabiki. Lakini bila shaka yoyote ni imani kubwa sana kwake kutoka kwenye benchi la ufundi pia. Ameendelea kuwa chaguo la kwanza kwenye idara ya kiungo kila anapokuwa fiti.
Kama kuna idara ambayo Yanga imejaa watu, ni pamoja na eneo la kiungo, yupo Aziz KI, Feisal Salum, Zawadi Mauya na Sure Boy. Lakini Aucho na Yanick Bangala nao wanacheza eneo hilo hilo.
Aucho ni aina ya kiungo ambaye sifa yake kubwa inabaki kuwa moja tu. Pasi za uhakika, katika hili nakubaliana na mashabiki wanaomwita Daktari. Ni fundi haswa. Hana mambo mengi ni pasi kama rula kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili.
Lakini ukijaribu kuangalia kwenye ukabaji, bado humuoni Daktari huyu akikichafua kweli kweli. Ukijaribu kuona kwenye mashambulizi, humuoni pia Daktari huyu akijiongeza na kupiga pasi nyingi za mwisho.
Nadhani Yanga wanahitaji pia kuwa na plani B. Timu ikianza na Bangala, Sure Boy na Feisal unaona utofauti mkubwa sana. Sure Boy na Feisal wana uwezo mkubwa sana wa kukaa na mpira, kupunguza watu na pasi za kuzalisha mabao, nawaona kama madaktari wenye vitu vingi kuliko Aucho.
Kuna muda unahitaji watu wenye vitu vingi uwanjani. Yule Bangala ni mtu na nusu ndiyo maana kila nafasi akipewa, anafiti moja kwa moja. Aucho amebaki na jambo kubwa moja tu, kupiga pasi za uhakika.
Ukabaji wake sio wa uhakika, kasi yake sio ya uhakika pia. Wachezaji wa aina hii wanazidi kupotea duniani. Kiungo anapaswa kuwa na udambwi dambwi wa kutosha. Sio kupasia tu.
Yule Zawadi Mauya pale Yanga akiaminika, anaweza kuchangia vitu vingi pengine kuliko hata Aucho. Mauya anaweza kupambana sana kwenye kukaba pengine kuliko mtu yoyote yule kwenye eneo la Kiungo la Yanga.
Kila timu lazima iwe na Mbeba Maji mmoja, kila timu lazima iwe na Mvunja Kuni Mmoja. Nadhani Yanga wanahitaji Plani B kwenye timu yao na hasa eneo la kiungo.
Huwezi kuwa na kiungo ambaye sifa yake kubwa ni kupiga tu pasi za uhakika, lazima Daktari aongeze vitu. Lazima Daktari jezi ichafuke lazima Daktari akimbie sana uwanjani.
Feisal pamoja na kuwa ana faida kubwa sana kwenye timu akicheza nyuma ya mshambuliaji lakini ukimweka pale kwa Aucho, anakupa pia vitu vingi kuliko Daktari.
Pasi za uhakika utakupa, mabao utayapata hata kama sio mengi. Atakaba kweli kweli. Mambo mengine kibao. Daktari yeye kazi yake ni moja tu. Kupiga pasi! Mpira unabadilika sana. Kasi ya mchezo imeongezeka ni lazima uwe na watu wanaweza kwenye na mabadiliko hayo.
Bado Aucho ni mchezaji tegemezi ndani ya timu na ni mchezaji wa daraja la juu lakini anatakiwa kuongeza vitu. Anatakiwa kuongeza sifa ya pili. Kunatakiwa kuwepo Plani B. Sio mechi zote utashinda kwa kuwa na kiungo fundi wa pasi tu. Kuna muda unahitaji mtu mwenye uwezo wa kukaba tu. Kuna muda unahitaji kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kupoza mpira.
Watu wenye mambo mengi pale Yanga wapo lakini bado kocha ana imani kubwa sana na Aucho. Hawa ndio watu wanaoaminiwa zaidi duniani. Hawa ndio watu wenye 54% ya kuaminiwa na watu. Sio jambo dogo, wanastahili kupewa heshima.
Ukitazama uteuzi wa kocha wa Yanga, unagundua Bangala ndiye mchezaji muhimu zaidi kikosini. Kuna muda kocha anatamani kuwa na kina Bangala wawili. Mmoja acheze nafasi ya kiungo na mwingine aje nyuma kwenye ulinzi wa kati. Lakini ukitazama matumizi ya Aucho, yeye yuko pale pale.
Ni mzee wa pasi tu. Hakuna cha ziada. Mpira na hasa kwa mchezaji wa kiungo ni zaidi ya kupiga pasi. Hata upige pasi 200 kwa mechi moja, kama hakuna kinachofuata ni kazi bure.
Yanga lazima wawe na Plani B, sio kila mechi utashinda kwa kuwa na kiungo mpiga pasi tu. Wale kina Sure Boy na Mauya waongezewe idadi ya mechi. Wale kina Mauya na Sure waongezewe dakika za uwanjani. Kuna kitu kipya wataongeza. Kuna jambo kubwa wataleta.
Bado Aucho ni mchezaji mzuri lakini uwezo wake mkubwa uko kwenye kupiga pasi tu. Zipo mechi ambazo zinahitaji ubora huo tu lakini sio nyingi. Kiungo akiwa na vitu vingi, anafanya Boli litembee.