Mhasibu mbaroni madai kutekwa, kuporwa mil. 60/-




MHASIBU wa Kampuni ya Your Home Choice ya Keko, Dar es Salaam, Deodatus Luhela (35), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa na kujeruhiwa na majambazi kisha kuporwa Sh. milioni 60 za mwajiri wake.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP) Jumanne Muliro.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP) Jumanne Muliro, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa mtuhumiwa alitoa taarifa kituo kidogo cha polisi cha Gongo la Mboto na baadaye kufungua jalada katika Kituo cha Polisi Chang’ombe akidai kufanyiwa kitendo hicho.

Muliro alisema Novemba 14, mwaka huu, mtuhumiwa huyo katika taarifa alizotoa polisi, alidai kuwa majambazi walimjeruhi na kumpora Sh. milioni 60 alizokuwa ametumwa na mwajiri wake kuzichukua katika benki ya CRDB tawi la TAZARA.

Alisema Luhela alidai kuwa siku hiyo, saa 3:30 asubuhi, alikamatwa na majambazi wawili waliokuwa na gari jeusi baada ya kumtishia kwa silaha na baadaye akaingizwa kwenye gari.

Kwa mujibu wa Muliro, mtuhumiwa alidai kuwa majambazi hao walimjeruhi mkono wa kushoto na shavuni na hatimaye kumpora fedha zote alizokuwa nazo.


“Alidai kuwa baada ya tukio hilo alitupwa maeneo ya Gongo la Mboto njia panda ya Pugu na Mbezi, akajikongoja  hadi kituo cha Polisi ambako alipewa PF. 3 (Fomu namba tatu ya polisi)  kwa ajili ya matibabu.  Baadaye mtuhumiwa huyo alifungua kesi ya unyang’anyi na kuporwa Sh. milioni 60 katika kituo cha Polisi Chang’ombe,” alisema Muliro.

Baada ya taarifa hizo, Muliro alisema polisi walimhoji kwa kina na kubaini kuwa  taarifa hizo zilikuwa  za uongo.

Alisema ilipofika Novemba 15, saa 8:00 mchana, mtuhumiwa aliwaongoza askari hadi Chanika Kitunguu, jijini Dar es Salaam, alikokuwa ameficha fedha hizo.


POLISI FEKI MBARONI

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, limamshikilia Joseph James (32) mkazi wa Kijitonyama, Dar es Salaam, kwa kujifanya askari polisi  kutoka makao makuu ya upelelezi, Dodoma.

Kamanda Muliro alisema James amekamatwa baada ya ufuatiliaji kutokana na taarifa za kuwapo kundi la watu wanaojifanya polisi na kuwanyanyasa watu pamoja na kuwatishia kwa tuhuma mbalimbali za uongo.

“Uchunguzi umebaini mtuhumiwa huyu amekuwa akishirikiana na wenzake ambao wamekuwa wakitumia gari aina ya Subaru lenye namba za usajili T 550 DST alilokamatwa nalo,” alisema Muliro.

Kamanda alibainisha kuwa jeshi linawafuatilia watu wengine waliokuwa wakishirikiana naye wakijifanya askari polisi na maofisa wa usalama wa taifa ambao hukamata watu ovyo, kuzunguka nao mitaani kwa kutumia gari huku wakiwatishia kuwa watafikishwa katika vyombo vya dola na baadaye kuwataka watoe pesa ndipo wawaachie.


 “Jeshi la Polisi halikubaliani na hali hiyo. Ulinzi na ufuatiliaji wa mambo mbalimbali upo katika kiwango cha juu na yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kihalifu atakamatwa, atahojiwa kwa kina na baadaye atafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisisitiza.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad