Mjane wa Mengi Agonga Mwamba Matunzo ya Watoto




MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupa rufaa ya mjane wa aliyekuwa Mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi, Jackline Mengi iliyopinga kukataliwa matunzo ya wanawe wawili alioachiwa na marehemu mumewe.

Uamuzi huo ulitolewa mahakamani hapo Oktoba 24 mwaka huu mbele ya Jaji John Nkwabi na ulitokana na kile kilichosemwa kuwa Mahakama ya Watoto ya Dar es Salaam ya Kisutu ambako Jackline alipeleka mashitaka yake awali haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Jaji Nkwabi alisema Mahakama Kuu haiwezi kushugulika na rufaa hiyo kwa sababu ilitokana na shauri lililopelekwa katika mahakama isiyo na mamlaka hivyo inatupwa.

Aliieleza mahakama kuwa mrufani (Jackline) alipaswa kuanzisha madai yake kwa kuzingatia utaratibu na ushauri aliopewa katika Mahakama ya Watoto ya Kisutu wa kuwasilisha madai katika Mahakama ya Mirathi na Usimamizi wa Watoto badala ya mahakama hiyo ya watoto ya Kisutu, Dar es Salaam.


Wakili wa mrufani alidai kuwa mahakama hiyo ilifanya makosa ya kisheria kwa kutothibitisha madai hayo ambayo yalikubaliwa na wasimamizi wawili wa mirathi ya marehemu Mengi ambao ni Abdiel Mengi na Benjamin Mengi.

Katika hukumu ya Mahakama ya Kisutu iliwekwa wazi kwamba mahakama ya mirathi ndiyo yenye mamlaka, hoja ambayo iliungwa mkono katika uamuzi wa Jaji Nkwabi.

Katika mahakama ya Kisutu, mrufani aliomba malipo kadhaa yakiwemo malimbikizo ya matunzo ya zaidi ya Sh milioni 401.9 kwa watoto wawili, zaidi ya Sh milioni 94.3 za ada ya shule za kuanzia Agosti mwaka jana hadi Julai mwaka huu.

Nyingine ni malipo ya kiasi hicho cha ada ya shule kwa kipindi cha kuanzia Agosti mwaka huu hadi Julai, 2023 na gharama nyingine za shule kila mwaka hadi watoto watakapomaliza masomo ya kidato cha sita.

Pia aliomba malipo ya shilingi milioni 24 kwa ajili ya usafiri wa shule kwa watoto hao kuanzia Januari hadi Desemba mwaka huu na miaka yote hadi watoto watakapomaliza kidato cha sita sambamba na malipo ya bima ya matibabu ya Sh milioni 30 kwa mwaka hadi watoto watakapofikisha miaka 18.

Mbali na hayo alitaka malipo ya Sh milioni 15 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya nyumba hadi watoto watakapofikisha umri wa miaka 18 na zaidi ya milioni 36 kwa ajili ya bima ya nyumba hadi watoto hao watakapofikisha miaka 18.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad