Mke wa Rubani "Mume Wangu Amekufa Kifo cha Maumivu Makali"




Nairobi,Kenya. Mapema Jumapili asubuhi, Fiona Ndila Mutuka anaondoka nyumbani kwake katika eneo la Ngong na kuelekea Mtito Andei ambayo ni umbali wa takribani kilomita 253 kutoka mji huo.

Anamuaga kwa busu mtoto wake wa miaka sita, Leon na kuanza safari yake.

Fiona amekata tiketi ya treni ya Madaraka inayoondoka saa 2.00 asubuhi. Wakati akielekea stesheni anazungumza kwa njia ya simu na mume wake Peter Omondi Odhiambo, aliyekuwa rubani wa ndege ya Precision Air iliyoanguka Novemba 6 mwaka huu. Hiyo ilikuwa ni saa 11.53 alfajiri.

Mumewe anamuulizia kuhusu mtoto wao na mambo mengine ya kifamilia. Mengi walizungumza usiku wa jana yake kwa hiyo Peter anaifahamu safari ya mkewe halkadhalika Fiona anafahamu kuwa asubuhi hiyo mumewe alikuwa na safari ya kuelekea Bukoba.


“Safe Skies” ndilo neno humwambia mume wake kumtakia safari njema kila wanapoagana. Peter naye anamuaga kwa kumtakia safari njema mkewe.

Fiona anawasili Mtito Andei saa 4.45 asubuhi na anapofungua simu kuangalia mitandao ya kijamii anakutana na habari ya ajali ya ndege ya Precision Air iliyoanguka Ziwa Victoria kutokana na hali mbaya ya hewa.

Huku moyo ukimuenda mbio alianza kuwapigia simu ndugu na jamaa kujihakikishia alichosikia. Wa kwanza alikuwa Alex Odhiambo ambaye ni kaka mkubwa wa Peter. Hakuwa na taarifa yoyote. Akampigia dada yake Getrude Achieng naye pia hakuwa na taarifa.


Akarudi kwenye mtandao wa WhatsApp kuangalia ‘Last seen’ ya mume wake, akaona mara ya mwisho ni muda ule walipoongea wakati akianza safari. Akajipa moyo “ataokolewa”.

Saa 9 alasiri alipigiwa simu na ofisa rasilimali watu wa Precision Air akimjulisha kuwa ndege imeanza kutolewa katika eneo la ajali hata hivyo hakumueleza iwapo mumewe ni mmoja wa manusura au la.

Ilichukua saa tisa zaidi kabla familia haijajulishwa kuhusu kifo cha Peter. Taarifa hiyo alipewa kaka wa Peter kupitia ofisi ndogo ya shirika hilo iliyopo Nairobi.

Kwa Fiona habari mbaya alianza kuinusa mapema baada ya kuona mmoja wa marafiki wa mume wake ambaye naye ni rubani, akiwa ameweka picha ya Peter katika profile ya WhatsApp.


“Ukiacha hiyo, nilipoona picha ya ndege ikiwa ndani ya maji nilihisi tu nitapokea habari mbaya kwasababu Peter hakuwa akijua kuogelea,” anasema Fiona na kuongeza:

Mume wangu amekufa kifo cha maumivu makali sana, moja ya vitu alikuwa anataka kujifunza ni kuogelea lakini bahati mbaya hakuweza kuitimiza ndoto hiyo.”

Anasema Peter alikuwa amepanga kurudi nyumbani kwake Novemba 23 kwaajili ya kuhudhuria mahafali ya mtoto wao ambayo yangefanyika siku inayofuata.

Peter ambaye angetimiza miaka 45 mwezi ujao, anatajwa na marafiki zake kuwa alikuwa mtu wa watu, asiyekubali kushindwa na aliyekufa akifanya kile alichokuwa akikipenda zaidi….urubani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad