Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ikiwa angani
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mussa Mbura amesema sababu ya ndege ya ATCL kushindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba ni mvua mkubwa na ukungu uliokuwa umetanda katika eneo hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Amesema ndege hiyo iliyotakiwa kutua leo saa 12:05 mchana, ilikumbana na changamoto hiyo ya hali mbaya ya hewa kiasi cha kumlazimu rubani kwenda kutua katika uwanja wa ndege wa Mwanza.
Ameongeza ndege hiyo ilikuwa mbali kwamba haijaanza kutua pindi rubani alipoamua kuchukua hatua hiyo.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa ni ndege hiyo pekee ilishindwa kutua na kuongeza kuwa sasa hali ni shwari na ndege zinaendelea kutua hivyo hakuna ndege iliyozuiliwa kutua katika uwanja huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mussa Mbura
Kauli hiyo ya TAA imekuja saa chache baada ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Neema Lugangira kueleza kwamba ndege aliyoipanda leo imeshindwa kutua katika uwanja huo wa Bukoba.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mbunge huyo ameandika “Still shaken lakini Mungu ni Mwema. Nimepanda ndege asubuhi ya leo kwenda Bukoba. Safari ilikuwa na changamoto, tumefika lakini ndege ikashindwa kutua. Nampongeza Rubani kwa uamuzi sahihi wa kurudi Mwanza na sasa narudi Dar. Serikali ibebe kwa uzito suala la airport mpya Bukoba.”